ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk. Benson Bagonza amezungumzia kauli za viongozi wawili, Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Job Ndugai. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).
Ni baada ya kutoa lugha tofauti kuhusu Serikali kukopa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Rais Samia alisema, Serikali anayoingoza itaendelea kukopa ili kukamilisha miradi iliyopo na kuanzisha mipya kwa manufaa ya Taifa ili kuchochea maendeleo.
Alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku takribani mbili kupita tangu, Spika Ndugai kusema, umefika wakati nchi ikaachana na utaratibu wa kukopa na kutumia fedha za ndani kama tozo kugharamikia miradi hiyo kwani madeni yakizidi yanaweza kusababisha nchi kupigwa mnada.
Baada ya kauli za viongozi hao, Askofu Bagonza ametumia ukurasa wake wa kijamii wa Facebook, kuzichambua, akianza kwa kusema;
Umoja au Uhuru wa Mihimili?
Spika kakosoa.
Rais kajibu.
Nani yuko sahihi?
Ugumu uko hapa:
1. Ukiishakuwa kiongozi unapoteza haki ya kulalamika. Rais kaonyesha uongozi kwa kukopa. Spika kapoteza uongozi kwa kulalamika.
2. Tunahitaji uhuru wa mihimili siyo umoja wa mihimili. Maslahi ya walipa kodi yapo katika uhuru wa mihimili si umoja wa mihimili.
3. Watawala wasipigane vijembe. Simba akinguruma anamsaidia mwindaji ajue mahali Simba alipo. Rais azingatie moyoni.
4. Spika kapatia kutujulisha hatari za mikopo. Atujulishe na hatari ya kulipa mishahara wasio wabunge. Amalizie kutujulisha uhalali wa sheria zinazotungwa na wasio wabunge.
5. Mikopo ikisababisha nchi ipigwe mnada, bunge na mahakama watakosa uhalali wa kutumia sheria zilizotungwa na wasio wabunge.
6. Spika anashabikia tozo kuliko mikopo. Tozo ni maumivu yetu. Zimeua matumaini ya kuishi ili tuweze kwenda madarasa yanayojengwa na tozo.
7. Tukumbushane: Wakikosekana wapinzani wa kweli, CCM itatengeneza wake wa ndani. Tumempata Kiongozi Mkuu wa upinzani bungeni. Mmemwona? Vaeni miwani.
CCM imara inahitaji Upinzani Imara siyo upinzani wa ndani.
Kazi Iendelee.