Sakata la wachezaji Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya na Aggrey Morris waliosimamishwa na klabu ya Azam FC limefikia patamu, kufuatia uongozi wa klabu hiyo kutoa kauli nzito.
Wachezaji hao watatu walisimamishwa mwezi Septamba kwa utovu wa nidhamu kwa muda usiojulikana, huku ikidaiwa huenda wakaachwa jumla na klabu hiyo ya jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Soka wa Azam FC Jonas Tiboroha amesema wachezaji hao huenda wakaondolewa jumla kwenye kikosi na kupewa nafasi ya kujiunga na klabu nyingine ndani ama nje ya nchi.
Amesema katika kipindi hiki ambacho wanaendelea kutumikia adhabu, Azam FC inaendelea kuwalipa mishahara kama kawaida, lakini Benchi la Ufundi chini ya Kocha Mkuu kutoka Zambia George Lwandamina halina habari nao tena.
“Sidhani kama Sure Boy, Mudathir na Aggrey watakuja kucheza tena Azam, kocha hana mpango nao tena na sisi kama viongozi hatuna habari nao japokuwa wana mikataba ya kuendelea kuitumikia Azam. Tunaendelea kuwalipa mishahara yao kama kawaida mpaka itakapotamatika.” amesema Jonas Tiboroha
Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya na Aggrey Morris ni miongoni mwa wachezaji wakongwe waliobaki kwenye klabu ya Azam FC, na baadhi ya wadau wa soka nchini wamekua wakiamini kukosekana kwao kwenye kikosi, huenda ikawa sababu ya timu hiyo kusuasua katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Azam FC inashika nafasi ya sita kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 10, baada ya kucheza michezo saba ya Ligi hiyo msimu huu 2021/22.