Mbunge wa kuteuliwa Humphrey Polepole (CCM)
SAA chache baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kukisimamisha kwa muda kipindi cha ‘Shule ya Uongozi’ kinachoendeshwa na Mbunge wa kuteuliwa Humphrey Polepole (CCM), kiongozi huyo amesema hiyo ni mitihani midogo kwake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mbunge huyo ambaye ndiye mmiliki wa Televisheni ya Online ya ‘Humphrey Polepole Online’ iliyokuwa inaanda kipindi hicho, amesema anatarajia kukaa na timu yake ya wasaidizi ili kuona namna ya kujinasua katika adhabu aliyopewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Aidha, amejinasibu kuwa kazi ya kusema kweli bado ina safari na yeye hatokata tamaa maadam anachokifanya kinalinda masilahi mapana ya nchi, watu, mamlaka ya nchi na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Polepole ametoa kauli hiyo leo tarehe 17 Disemba, 2021, baada ya Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutangaza kukisimamisha kwa muda kipindi hicho cha ‘Shule ya Uongozi’ kinachorushwa na Huphrey Polepole Online Television kutokana na kukiuka misingi ya sheria na kanuni za huduma ya utangazaji.
Uamuzi huo umetangazwa na kamati hiyo jijini Dar es Salaam baada ya kumhoji Mbunge huyo kuteuliwa ambaye ndiye mmiliki wa televisheni hiyo na mwendeshaji wa kipindi husika kinachoruka kupitia mitandao ya kijamii.
Kamati imetoa masharti ya kipindi hicho kufunguliwa ambapo sharti la kwanza ni kituo hicho kuwa na watumishi wenye taaluma ya uandishi na utangazaji wa habari ili kuleta tija katika vipindi vyake.
Awali kamati imeeleza kwamba televisheni hiyo haina watumishi wenye taaluma husika hivyo kupelekea kukiuka sheria, misingi na kanuni za taaluma husika.
Pia, kamati hiyo imemuagiza kuhakikisha vipindi vyake vyote vinazingatia sheria, kanuni na misingi ya uandishi na utangazaji wa habari pamoja na masharti ya leseni yake.
Baada ya kutimiza masharti hayo, kituo hicho kitatoa taarifa kwa TCRA, ambapo ikijiridhisha kuwa maelekezo yote yamezingatiwa, kipindi cha Shule ya Uongozi kitarejea na kuwa chini ya uangalizi wa mamlaka hiyo kwa miezi sita.
Kituo hicho pia kimepewa onyo kali baada ya kuthibitika kuwa maudhui ya kipindi ni ya upotoshaji yanayoweza kusababisha taharuki kwa wananchi.
Katika vipindi tofauti Polepole amekutwa na hatua kwa kusema kuwa virusi vya UVIKO-19 vimetengenezwa na kampuni kubwa ili kuuza chanjo na kujipatia fedha, madai ambayo hakuweza kuyathibitisha na hakutoa nafasi kwa mtaalam wa afya kutoa ufafanuzi wakati akiendesha kipindi hicho.
Kamati imeeleza zaidi kuwa madai hayo yanadhoofisha jitihada za mapambano dhidi ya ugoinjwa huo.
Pia amekutwa na hatia ya kusema deni la Taifa limekuwa kubwa na kuwataka viongozi kutoa ufafanuzi lakini hapakuwa na kiongozi kwenye kipindi kutoa ufafanuzi huyo.
Aidha, kamati imethibitisha kuwa mawaziri wa fedha walitoa ufafanuzi bungeni kuhusu deni na kusema kuwa ni himilivu.
Akifafanua hukumu hiyo, Polepole amesema alipata nafasi ya kusikilizwa.
“Kazi ya kusema kweli ina safari kidogo anadhani kwa mimi ambaye ni mwanachama wa CCM kwa imani na ninayeamini katika kusema kweli daima bila kuweka chembe ya fitina ndani yake… na ninayemini katika ahadi nyingine ya mwanachama wa CCM inayosema nitafanya jitihada kujielimisha na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote, kwangu mimi hii ni mitihani midogo.
“Nitakaa na wasaidizi wangu nitatafakari hukumu hii iliyotolewa leo, na nitawajulisha hatua ambayo itafuata,” amesema.