Balozi Khamis Kagasheki
WAZIRI wa zamani wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Balozi Khamis Kagasheki amezungumzia kile kinachoendelea kwa Mbunge wa Kuteuliwa, Humphrey Polepole na kilichofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).
Hivi karibuni, Kamati ya Maadili ya TCRA ilitangaza kusimamisha kipindi cha ‘Shule ya Uongozi’ kilichokuwa kikirushwa na channel ya mtandaoni ya Humphrey Polepole kutokana na kutokukidhi matakwa.
Aidha, wakati TCRA ikimshushia nyundo hiyo, Kamati Kuu ya chama chake- Chama Cha Mapinduzi (CCM), ilitoa taarifa ya kumwita yeye na wabunge wenzake, Jerry Silaa wa Ukonga na Askofu Josephat Gwajima wa Kawe kuhojiwa juu ya tuhuma zinazomkabili.
Kwa pamoja, watakuwa wanahojiwa mara ya pili ndani ya chama hicho, wakitanguliwa kuhojiwa na kamati ya maadili ya wabunge wa CCM.
Balozi Kagasheki aliyewahi kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), juzi Jumatatu, tarehe 20 Desemba 2021, alitumia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kuzungumzia kile kinachomtokea Polepole huku akiinyooshea kidole TCRA.
Humphrey Polepole
Ujumbe wenye huu hapa;
Humphrey siyo rafiki yangu. Pia siyo adui yangu. Sikuwahi kuketi popote na yeye kwa maongezi. Mara moja tu niliongea nae kwa simu kuhusu jambo lililo mhusu mwanachama mwenzetu na Boss wake (Bashiru) alikuwa kalivalia njuga.
Inasemekana zipo tuhuma zinazo mkabili na chama chetu hakijatoa hukumu dhidi yake mpaka kisikie utetezi wake. Kingeweza kumchukulia hatua bila hata kufuata taratibu kama tulivyo ona huko nyuma.
Najiuliza, TCRA kabla ya hatua zao dhidi ya Polepole, walimpa fursa ya kujieleza? Alisikilizwa? Alisema nini?
Nimeusikiliza mlolongo wa tuhuma dhidi yake lakini nikazidi kujiuliza ‘na ikawaje akapewa leseni?’ Vitu vingine TCRA ilipaswa ivijue kabla ya kutoa leseni.
Pamoja na yote “Darasa” lake halikuwa hewani siku moja au mbili kwa uchache wa siku, kweli TCRA walikuwa bado tu hawajaona kwamba leseni yao haikuwa katika mikono salama? Niwambie tu, TCRA mnachekesha.
Huu uadilifu mnaupata wapi. Awamu ya tano mmetoa leseni kwa so-called wanaharakati huru wakitukana, kudhalilisha wazee na wastaafu wa Taifa letu. Mpo kimya.
Maongezi ya Watanzania yamedukuliwa na kuwekwa hadharani. Mpo kimya. Leo mnasimamia maadili. Really? Mimi simtetei Humphrey kama Humphrey. Kuna maswala ya msingi ambayo ni zaidi ya mtu.