Dodoma. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiwa kimemuweka kiporo mbunge wa kuteuliwa Humphrey Polepole, yeye ameandika tena kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba, CCM pekee ndiyo inaweza kukabiliana na wahuni.
Mbali na Polepole, waziri wa zamani wakati wa Serikali ya awamu ya nne, Balozi Khamis Kagasheki, naye kwenye ukurasa wake wa Twitter ameandika kwa kirefu kumzungumzia Polepole.
Kati ya mengi aliyoandika, Kagasheki alisema awali kulikuwa na leseni zilizotolewa kwa watu waliojiita wanaharakati huru waliokuwa wakitukana, kudhalilisha wazee na wastaafu wa Tanzania na hawakuchukuliwa hatua, lakini inashangaza hivi sasa Polepole kashughulikiwa.
Mwananchi jana lilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari azungumzie hoja za Balozi Kagasheki.
Dk Bakari alisema Kagasheki ana uhuru wa kuzungumza, hivyo yeye kama mkurugenzi hawezi kumsemea.
“Nafikiri yeye ndiye mwenye majibu mazuri, ukimuuliza yeye atakuambia kwa kina kwa nini ameandika, ukiniuliza mimi unaniwekea maneno yake,” alisema Dk Bakari.
Kuhusu udhalilishaji uliokuwa ukifanywa na waliokuwa wakijiita wanaharakati huru, alisema kama kuna makosa yalikuwa yanafanyika ipo Sheria ya mwaka 2015 inayofanya kazi.
“Wamekuwa wakiripoti polisi wanaofanyiwa udhalilishaji na kuna vitu vinaendelea huko (polisi),” alisema Dk Bakari.
Haya yanatokea ikiwa ni siku chache tangu mkutano wa Kamati Kuu ya CCM uliofanyika Desemba 17, 2021 Ikulu Chamwino jijini Dodoma, chini ya Mwenyekiti Rais Samia Suluhu Hassan kuazimia kuwaita wanachama wake watatu ambao ni Polepole, mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa na mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima ili wajieleze mbele ya kamati hiyo kutokana na tuhuma zinazowakabili.
Hata hivyo, jana Polepole kwenye ukurasa wake wa Twitter aliandika:
“Kitu kimoja nina hakika ni kwamba wahuni hawatashinda, lakini kitu kimoja nina imani kubwa sana ni kwamba ni Chama cha Mapinduzi (CCM) pekee ndio kina uwezo wa kitaasisi na kidhamira wa kukabiliana na wahuni. Kazi ni kwetu wana CCM.”
Polepole amekuwa akitumia neno ‘wahuni’ kuwaita watu anaodai wanaweka mbele masilahi binafsi.
Mbunge huyo kuna wakati alifafanua neno ‘wahuni’ akisema amelitumia kuwakilisha watu wanaotanguliza maslahi yao mbele badala ya masilahi mapana ya taifa.
Polepole alikuwa na kipindi chake cha Shule ya Uongozi kilichokuwa kikirushwa mtandaoni.
Kipindi hicho cha Shule ya Uongozi tayari kimefungiwa kwa muda usiojulikana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa makosa matatu ya kutoa taarifa ya upotoshaji kuhusu chanjo ya Uviko-19.
Pia, kutoa maneno ya uongo na udhalilishaji kuwa viongozi wengi waliopo katika Serikali ya Awamu ya Sita ni waoga kusema ukweli kuhusu deni la taifa.
Kagasheki alaumu TCRA
Katika ukurasa wa Twitter, Balozi Kagasheki alitoa maelezo marefu kuhusu Polepole, huku akiitupia lawama TCRA kwa kuchelewa kuchukua hatua.
Kagasheki ni waziri wa zamani wa maliasili na utalii na mbunge wa zamani wa jimbo la Bukoba Mjini (CCM), kwenye ukurasa wake huo alisema;
“Humphrey @hpolepole siyo rafiki yangu. Pia siyo adui yangu. Sikuwahi kuketi popote na yeye kwa maongezi. Mara moja tu niliongea naye kwa simu kuhusu jambo lililomhusu mwanachama mwenzetu na Boss wake (Bashiru) alikuwa kalivalia njuga. Inasemekana zipo tuhuma zinazomkabili na chama chetu hakijatoa hukumu dhidi yake mpaka kisikie utetezi wake.
“Kingeweza kumchukulia hatua bila hata kufuata taratibu kama tulivyoona huko nyuma. Najiuliza, TCRA kabla ya hatua zao dhidi ya Polepole, walimpa fursa ya kujieleza? Alisikilizwa? Alisema nini?” alihoji.