CHUNGU na tamu kwa mashabiki wa Simba kuelekea mechi yao na KMC, itakayopigwa kesho, Ijumaa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Ipo hivi; kitakachowafurahisha mashabiki wa Simba ni kupona kwa mastaa wao waliokuwa wanaumwa mafua ambao ni Jonas Mkude na Hassan Dilunga kwani afya zao zimeimarika, hivyo wanaweza wakakipiga dhidi ya KMC.
Lakini kwa upande wa nahodha wao, John Bocco bado anaumwa pamoja na Larry Bwalya makocha walikuwa wanamuangalia kwa mazoezi kuamua kama anafiti kwa ajili ya mchezo huo, wakati Bernard Morrison amesafiri kwenda nchini kwao, Ghana.
Kukosekana kwa Morrison na Bocco wadau wa soka wamezungumzia kwamba nafasi zao zinaweza kuzibwa na Meddie Kagere mwenye mabao manne na Dilunga ambaye alikuwa anaumwa, ila amepona.
Beki wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa alisema japokuwa Morrison ni injini ya timu kulingana na mechi alizocheza kwa msimu huu, wachezaji waliopo kikosini wanaweza wakaipa timu matokeo.
“Tayari upande wa washambuliaji yupo Kagere ambaye ana mabao manne ingawa Morrison alihusika zaidi kwenye mabao hayo. Ila nafasi yake anaweza akacheza Dilunga ambaye naye yupo kwenye kiwango kizuri,” alisema Pawasa.
Mlinzi wa zamani wa timu hiyo, Lubigisa Madata alisema ilimradi kocha Pablo Franco alikuwa anajua mapema kukosekana kwa mastaa hao atakuwa ameandaa mbinu mpya za kuwakabili KMC kulingana na kikosi kilichopo.
“Ingawa kukosekana kwa Morrison kutakuwa na pengo kidogo kutokana na mchango wake kwenye timu, ila kwa Bocco kakosa mechi nyingi na bado Simba ilishinda,” alisema Lubigisa.
Kikosi kimetua jana Jumatano mkoani Tabora kikiwa na mastaa 24.