CCM: Mazingira ya kisiasa yako sawa




KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema mazingira ya siasa nchini yapo sawa, lakini tatizo kubwa ni nchi kugeuzwa kuwa sehemu ya kampeni baada ya uchaguzi kumalizika.

Chongolo alitoa kauli hiyo jana alipojibu maswali yaliyoulizwa na waandishi wa habari katika mkutano wa kuelezea mafanikio ya taifa katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.

"Mimi ninaamini mazingira ya siasa yapo sawa nchini kwa sababu hakuna mtu ambaye amezuiwa kufanya kampeni wakati wa kampeni unapofika, lakini tuna changamoto kama nchi na changamoto hii ni kubwa sana. Ngoja niseme kidogo, tunataka kuigeuza nchi kuwa ni nchi ya kampeni na siasa.

"Kwamba tunapoanza kuanzia tarehe moja ya uchaguzi tunaruhusu leo kuanza kampeni za uchaguzi, tunaenda kwenye kampeni, watu wanachaguliwa, tukimaliza kampeni tunaanza kuwasema waliochaguliwa mpaka tunapokuja tena kwenye kampeni za uchaguzi mwingine.

"Hatuwezi kuwa na nchi ya namna hiyo, niambie ni nchi gani duniani chama cha siasa kinapoanguka kwenye uchaguzi kinaanza kuwa na 'platform' nyingine za kila siku kuhangaika na waliochaguliwa au kuhangaika na siasa," alisema.


 
Alisema CCM inaposimama kuzungumzia umuhimu wa miaka hii 60 ya uhuru, inazungumzia suala ambalo wana wajibu nalo kwa asilimia 100, ikizingatiwa chama hicho kimepewa dhamana ya kuongoza nchi, kuunda serikali na kusimamia dola kuanzia kupigania uhuru.

Alisema kwa sasa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinatolewa katika hospitali 12 za ubingwa daraja la juu; upasuaji mkubwa wa moyo, huduma za usafishaji na upandikizaji wa figo, matibabu ya kisasa ya saratani na matibabu ya mifupa yanatolewa nchini.

Alikumbusha kuwa mwaka 1961 hakukuwa na jaji Mtanganyika hata mmoja katika mahakama zote lakini sasa majaji wote ni Watanzania.


Chongolo alisema kumeshuhudiwa pia kuanzishwa na kuimarishwa vyombo mbalimbali vya kusimamia utawala bora kama vile Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Sekreterieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kuhusu elimu, Chongolo alisema idadi ya shule za msingi zimeongezeka kutoka 3,270 mwaka 1961 hadi 18,546 mwaka 2021. Wanafunzi wameongezeka kutoka 486,470 mwaka 1961 hadi kufikia 11,196,788 mwaka 2021 na walimu wameongezeka kutoka 9,885 mwaka 1961 hadi 197,929 mwaka 2021.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad