CCM wamkalia ‘kooni’ Spika Ndugai



SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameendelea kukaliwa ‘koo’ na chama chake baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Singida kusema, hakitakubali kuona mtu yoyote anapingana na Rais Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Mwandishi Wetu, Singida … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, tarehe 30 Desemba 2021 na Mwenyekiti wa CCM, mkoa huo Alhaji Juma Kilimba wakati anazungumza na waandishi wa habari, akimpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya tangu aingie madarakani.

Hivi karibuni, Spika Ndugai alisema, umefika wakati wa kuanza kutekeleza miradi kwa fedha za ndani ikiwemo tozo jambo ambalo Rais Samia alisema, serikali itaendelea kukopa kugharamikia miradi hiyo ya maendeleo.

Alhaji Kilimba ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) amesema, “Sisi kama CCM na kulingana na Ilani yetu, moja ya kazi ni kuwahudumia wananchi ili ikifika miaka mitano, tuwaeleze tumefanya kwa kiwango gani na mkataba huu anatuongoza Rais Samia.”


 

Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM
“Hizi kelele za kukatisha tamaa zimekuwepo kuwa kwa nini tunaendelea kukopa, kwa nini tunakopa, tusitumie fedha za ndani, lakini wanazuoni wamesema, wengine na sisi CCM bado tunaamini nchi inajengwa kwa misingi mbalimbali ikiwemo mikopo,” amesema

MNEC huyo amesema, “kumkatisha tamaa Rais kuwa kwa nini anakopa, hata watangulizi wake wamekopa, deni tulilonalo sasa hivi la Sh.1.3 trilioni ni la kawaida sana, sisi kama CCM na mjumbe wa Halmashauri Kuu, tunamuunga mkono Rais Samian aendelee na kila jambo tunaloliona lina tija tupo na yeye na hii habari ya kukatishwa tamaa, tunaliona halina mashiko.”

Katika kusisitiza hilo, Alhaji Kilimba amesema, “kwa sababu Rais anafanya kazi aliyopewa na CCM na CCM ndiyo ilimpa Ilani na mimi naamini wa-NEC wenzangu wataniunga mkono kwamba hatutakubali wale wanaomkatisha tamaa wa ndani au nje, Rais afanye kazi.”



Job Ndugai
Alhaji Kilimba ameungana na CCM Mkoa wa Dar es Salaam, ambao nao kupitia kwa Mwenyekiti wake, Kate Kamba wamempongeza Rais Samia kwa kazi nzuri anayoifanya ikiwemo suala hilo la mikopo.

Kate alisema, hakuna asiyefahamu umuhimu wa mikopo na wanaopinga suala hilo hawajui thamani ya kukopa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad