Chanjo corona kutolewa makanisani Krismasi



MGANGA Mkuu wa Manispaa ya Singida mkoani Singida, Dk. Anuary Milulu, amesema watatumia siku ya Sikukuu ya Krismasi kutembelea nyumba za ibada, masoko, magulio na nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kupewa chanjo ya UVIKO-19.

Dk. Milulu aliyaeleza hayo kupitia mkutano wake na wataalamu wa afya katika wilaya hiyo jana muda mfupi kabla ya kuanza kutembea mtaani kuwafuata wananchi ili kuwapatia chanjo ya UVIKO-19 katika kampeni inayoendelea.

Alisema kuwa malengo ya Manispaa hiyo ni kuchanja watu 360 kwa siku katika kutimiza lengo la serikali la kuchanja watu 80,000 hadi 100,000 kwa siku.

Malengo hayo yanatekelezwa kupitia kampeni ya ‘Kuhamasisha Utoaji wa Chanjo ya UVIKO-19 katika Mpango Shirikishi na Harakishi Awamu ya Pili’ unaoendelea kutekelezwa nchini nzima.

Dk. Milulu alisema kupitia mkesha wa Sikukuu ya Krismasi watahakikisha wanawafuata waumini kwenye nyumba za ibada kwa lengo la kufikia watu 3,000 kwa mkoa wa Singida.


 
"Tumekutana na wataalamu hapa kupeana mbinu za kwenda kutoa chanjo kwa wananchi ili kufikia lengo la serikali. Njia mojawapo ni kutumia magari ya matangazo, hivyo wakati huu wataongeza idadi ya magari ili kuwafikia watu mbalimbali.

Alisema wamejipanga kuchanja watu 360 na awali walikuwa wakichanja watu 100 na mkakati walioweka utawezesha kufikia watu wengi zaidi.

"Hii ni mbinu tu ya kuwafikia hawa watu, tunaamini tukienda na kuwafikia watu tutachanja wengi zaidi," alisema Dk. Milulu.


Mtaalamu wa Ufuatilia na Udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, aliwataka maofisa hao kuwafuata wananchi nyumbani, shambani, ibadani na maeneo mengine ambako wanapatikana.

Alisema lengo ni kufikia malengo ya serikali kwa kuwafuata watu mahali walipo ili wapate chanjo ya UVIKO-19.
Alisema vikwazo vingi vinaweza kutatulika kwa kushirikiana kwa pamoja katika kuendesha kampeni hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad