Clatous Chama Amaliza Utata "Sifikirii Kurudi Tanzania"




Kiungo Mshambulaiji kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama amemaliza utata wa kurejea nchini Tanzania wakati wa Dirisha Dogo la usajili ambalo rasmi litafunguliwa Desemba 15.

Chama anahusishwa na taarifa za kuwaniwa na klabu za Simba SC na Young Africans zote za Jijini Dar es salaam.

Chama amemaliza utata wa sakata hilo alipohojiwa na Mtangazaji Diva kwenye kipindi cha Lavi Davi kinachorushwa na Wasafi FM.

Chama amesema hafikirii suala la kurudi nchini Tanzania, na kwa sasa ni mapema mno kuzungumzia safari yake ya kurejea katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ameitumikia kwa misimu mitatu mfululizo.


 
Amesema kwa sasa ni mchezaji halali wa RS Berkane na hana budi kujikita katika uwajibikaji ndani ya klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

“Siwezi kusema lolote kuhusu hilo, kwa sasa mimi ni mchezaji wa RS Berkane, sina budi kujizatiti katika majukumu yangu kwenye klabu hii.” amesema Chama

Hata Hivyo amekiri kuyakumbuka mazingira ya Tanzania na soka lake kwa ujumla, huku akimtaja Beki wa Kulia wa klabu ya Simba Shomari Kapombe kama rafiki yake wa karibu ambaye kila kukicha amekua akimkumbuka kutokana na walivyoishi wakati wote akiwa Simba SC.


“Kuna mambo mengi ninayakumbuka hapo Tanzania, maana niliishi na viongozi na wachezaji wa Simba SC vizuri, hata mashabiki nao niliishi nao vizuri, kuna mambo mengi sana ninayakumbuka kwa kweli,”

“Kuhusu mchezaji ambaye ninamkumbuka sana ni Shomari Kapombe, kwa sababu tuliishi chumba kimoja tukiwa kambini Simba SC, kuna mengi sana ambayo ninamkumbuka Kapombe, pia ninawakumbuka wachezaji wengine wa klabu ya Simba na viongozi pia.”

Chama aliuzwa RS Berkane ya Morocco mwezi Agosti mwaka kwa zaidi ya Sh700Milioni.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad