Dereva Asimulia Alivyonusurika Ajali iliyoua 10 Iringa



Iringa. Dereva wa akiba wa gari aina ya Hiace iliyopata ajali juzi eneo la Lungumba, Kata ya Mahenge mkoani Iringa na kupoteza maisha ya watu kumi, Hussein Ally amesema kilichookoa maisha yake ni kuruka kutoka kwenye gari.

Katika ajali hiyo watu wawili walinusurika, akiwamo Hussein.

Alisema awali alisikia kishindo cha kupasuka kwa tairi mojawapo la mbele na baadaye gari hilo likaanza kupoteza mwelekeo, ndipo alipofungua mlango na kuruka.

Katika ajali hiyo, Olivia Kadewele na watoto wake wawili ambao ni Benjamin Kadewele na Shutanite Kadewele waliokuwa wakielekea nyumbani kwao nchini Malawi kwa ajili ya likizo, walifariki papo hapo.


Mwingine aliyenusurika kwenye ajali hiyo ni Monica Philly, raia wa Malawi (wifi yake Olivia aliyefariki) ambaye amepoteza ujauzito wa miezi mitano.

Akizungumza na Mwananchi, Ally alisema yeye ndiye aliyeanza kuendesha gari hilo kutoka jijini Dar es Salaam na walipofika Mikumi mkoani Morogoro, alimkabidhi usukani mwenzake, Dickson Richard.

“Tulipofika maeneo ya Mahenge ghafla nilisikia kishindo kikubwa paaa! Hapo tairi moja lilikuwa limepasuka. Nikaona gari linapoteza mwelekeo hivyo nikaamua kuruka,” alisema na kuongeza:


“Nilitua chini vibaya nikajigonga, nimepata majeraha kichwani na kinachonitesa kwa sasa ni huu mguu, nasikia maumivu makali ila nilipoanguka nilijikokota mpaka barabarani, kuna bodaboda ilikuwa inakuja ikanichukua na kunipeleka Kituo cha Afya cha Mahenge,” alisema.

Manusura mwingine, Monica Philly alisema “Mimi sikumbuki kitu ila niliona tu gari linaenda porini baada ya kishindo kikubwa. Ndio nimejikuta hospitali,” alisema Monica ambaye mimba yake ya miezi mitano imeharibika.

Diwani aeleza walivyopona

Diwani wa Kata ya Mahenge, Shela Ngailo alisema saa 10 alfajiri walisikia kishindo cha gari kuanguka wakaenda eneo la tukio na kukuta ajali hiyo.

Alisema, gari hilo lilikuwa limeangukiwa na mti hivyo walisimamisha fuso na kulifunga kamba likauvuta mti na kuanza kuokoa watu, ambapo walipata miili tisa na majeruhi watatu waliowapeleka hospitali teule ya Ilula kwa ajili ya matibabu.

“Nguo za watu zilikuwa zimechanika sana, ilibidi nikimbie nyumbani nikachukue vitenge na kanga ili kuwasitiri. Mpaka sasa kichwa changu hakijatulia kabisa”.

Mume apoteza mke, watoto

Kati ya miili iliyotambuliwa ni wa mke na watoto wawili wa Shadrack Kadewele, raia wa Malawi na mkazi wa jijini Dar es Salaam. “Nilipopata taarifa nikaja, nimekuta mke wangu na watoto wawili wamefariki, naandaa miili ili nisafirishe kwenda Malawi,” alisema Kadewele.

Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk Iddy Omary alisema majeruhi wawili waliolazwa kwenye hospitali hiyo wanaendelea vizuri na matibabu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad