DPP aanza kufuta kesi za ugaidi Tanzania




MKURUGENZI wa Mashitaka ya Jinai nchini Tanzania (DDP), Sylvester Mwakitalu, amesema ofisi yake inaendelea “kuchambua na kupitia,” mamia ya majalada ya watuhumiwa wa ugaidi nchini, wakiwamo viongozi wa madhehebu ya Kiislamu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

“Ofisi yangu, inaendelea na uchambuzi kwa kesi zote wanazoita za ugaidi, kama ambavyo niliahidi wakati nilipoapishwa kushika nafasi hii. Tayari tumefanyia kazi baadhi ya majadala na waliokuwa wakituhumiwa wameachwa huru katika baadhi ya mikoa,” alisema Mwakitalu juzi Jumatatu.

Aliongeza: “Na hii si kazi ndogo. Nilipoingia ofisini, nilikuta zaidi ya majalada 100, tumekuwa tukichambua moja baada ya jingine. Tunaendelea kufanya hivyo na ambayo tutaona angalau yana ushahidi, tunaweza tukaendelea nayo mahakamani. Yale ambayo yataonekana ushahidi wake ni mdogo, tutafuta mashitaka.”

Mwakitalu alitoa kauli hiyo, akijibu swali la mwandishi, aliyetaka kufahamu hatua ambazo ofisi yake imezichukua, kushughulikia malalamiko ya wananchi, zikiwamo familia za viongozi hao wa dini ya Kiislamu.


 
Alitoa kauli hiyo, muda mfupi baada ya familia za mashekhe takribani 186 wanaodaiwa kuzuiwa katika magereza ya Ukonga na Segerea, Dar es Salaam, kwa zaidi ya miaka nane sasa, wanaotuhumiwa kwa makosa ya ugaidi, kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati mashauri yao.

Kuibuka kwa familia hizo, kumwomba Rais Samia kuingilia kesi za ndugu zao, kunatokana na wanachokiita, “upelelezi wa watuhumiwa hao, kuchukua muda mrefu bila kesi kusikilizwa.”

DPP Mwakitalu alisema ofisi yake, tayari imepitia majadala 30 hadi juzi, ambapo baadhi ya watuhumiwa wameonekana kesi zao hazina ushahidi wa kutosha na hivyo wameamua kuzifuta.


Alitaja baadhi ya maeneo ambako watuhumiwa wa ugaidi wamefutiwa kesi, ni Mwanza, Dodoma na Kagera.

Alisema: “Matarajio yangu ndani ya kipindi cha wiki mbili hadi tatu, tutakuwa tumemaliza kupitia majalada na kila kitu kitajulikana kwa wenye kesi za aina hiyo. Naomba wana familia za walioko gerezani, kuvuta subira.”

Juni 2021, Mkurugenzi huyo, aliwafutia mashitaka ya ugaidi mashekhe Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu kutoka Zanzibar, ambao kesi yao ilichukua takribani miaka minane.

Wakizungumza na waandishi wa habari juzi Jumatatu Dar es Salaam, wawakilishi wa familia hizo, walimwomba Rais Samia kuingilia kati, kutokana na kesi kuchukua muda mrefu bila kusikilizwa kwa madai kuwa “upelelezi haujakamilika.”


 
Kwa mujibu wa familia hizo, walituma barua karibu sita, kwa nyakati tofauti kwa Rais wa zamani, Hayati John Magufuli na Rais Samia Suluhu Hassan, ili kushughulikia malalamiko hayo, lakini barua hizo bado hazijajibiwa.

Abdulwahid Hamis Said, ndugu wa Swed Anuary Hatib, aliomba mamlaka husika zilifanyie kazi suala hilo, ili haki ya mashekhe hao itendeke.

“Tuna ndugu zetu 186 walio mahabusu ya Ukonga, wako takribani miaka minane hadi tisa, kesi zao bado hazijasikilizwa mahakamani. Ndugu yangu, ana takribani miaka tisa, kesi yake haijulikani.

“Tumekuwa tukifuatilia, lakini hatuambiwi kesi yao inasomwa lini. Tunapouliza, tunaambiwa hata miaka 300 itachukua, haitupi picha halisi,” alieleza.


Alisema, “nafahamu Serikali yetu ni sikivu, tunaiomba ione kuwa ina wajibu wa kusimamia sheria zake kama vile inavyotaka na wale wasimamizi wa sheria wawe waaminifu.

“Hatusemi waachwe huru tu, bali tunataka kama wana makosa basi waadhibiwe, lakini kama hawana hatia, waachwe huru,” alisisitiza.

Kiongozi Mwandamizi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Rajab Katimba, alisema kuna zaidi ya mashekhe 220, kati yao, 184 wako mahabusu na wanawake wawili wako gereza la Segerea kwa tuhuma za ugaidi.

“Hatupingi mashekhe kukamatwa, tunahoji kwa nini upelelezi haujakamilika kwa miaka hadi kumi. Upelelezi gani huo?” Alihoji Shekhe Katimba.

Zaujia Abdallah, ambaye hajui mahali alipo mumewe, Maulid Said Mbonde, aliyekamatwa Juni 2017, alimwomba Rais Samia aingilie kati, ajue hatima ya mumewe aliyemwachia watoto sita huku yeye akiwa hana uwezo wa kuwatunza.


 
“Sijui mume wangu yuko wapi. Alikamatwa tarehe 19 Juni 2017, akiwa kazini kwake Mwandege. Nimezunguka magereza yote, lakini sijamwona,” alieleza kwa sauti ya masikitiko.

Alisema: “Nami naomba Rais Samia anisaidie, maana hapa nilipo naumwa, nasumbuliwa na tatizo la mirija ya moyo kusinyaa na sina uwezo wa kufanya kazi ili kulea watoto hawa sita alioniachia.

“Maisha yangu yamekuwa ya shida, na naishi kwa hifadhi na kuombaomba kwa wasamaria wema, ili watoto hawa na mimi, tupate kuishi,” alisema.

Fatuma Nassoro, aliiomba Serikali ihurumie ndugu zao kwa kuwafikisha mahakamani ili hatima yao ifahamike. Alisema, kama wana hatia waadhibiwe, na kama hawana, waachwe huru.
Fatuma ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Zingiwa, Dar es Salaam, alisisitiza kuwa hana nia ya kuingilia uhuru wa Mahakama, bali mwito wao unatokana na mashauri hayo kuchukua muda mrefu.

“Mimi nina kaka zangu wawili, Ally Nassoro na Juma Zuberi, walikamatwa mwaka 2014, namaanisha mpaka sasa wana miaka minane hadi tisa, tangu wamekamatwa na kupelekwa mahakamani. Lakini ukienda mahakamani kufuatilia, unaambiwa kesi imeahirishwa kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

“Naomba Rais Samia, Mwenyekiti wangu wa chama, unisikilize na kilio hiki ni cha siku nyingi. Tulinyamaza kimya, tukidhani litafanyiwa kazi, lakini majibu hatuna. Tunakuomba Rais tuonee huruma kina mama wenzio,” aliomba Fatuma.

“Naomba hawa watu wapelekwe mahakamani, tutaelewa nini shida. Mimi ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Zingiziwa, nimepewa majukumu ya chama, nashindwa kuyatekeleza; nina watoto watatu na sita nilioachiwa na ndugu zangu, kiasi kwamba sina uwezo wa kuendesha familia.

“Nashindwa kutekeleza majukumu yangu ya kazi ya chama niliyokabidhiwa. Nina imani makatibu wa chama mtapata taarifa hizi na kuzifanyia kazi,” alisema.

Aisha Seleman, mke wa Zahak Rashid, aliye mahabusu tangu mwaka 2018, alimwomba DPP Mwakitalu, afanyie kazi malalamiko yao ili mumewe apate haki yake.

Alisema, “tunamwomba mwanamke mwenzetu Mama Samia, sikia kilio chetu pamoja na DPP na Mahakama, kuchukua jukumu katika hili ambalo ndugu zetu linawakumba.”

Hadija Mohammed Nkondo, mama mzazi wa Idd Seleman Nyange, aliyeko mahabusu tangu alipokamatwa mwaka 2015, aliomba aonewe huruma kwa kuwa ana watoto wao, ambao anadai haki zao zinakiukwa.

Hamid Haruna Mkanda, ambaye ndugu yake yuko mahabusu tangu mwaka 2015, aliyemtaja kwa jina la Abas Ayub Mkanda, alidai kuwa baadhi ya wazazi wamepata matatizo ya kiafya, kutokana na vijana wao kushikiliwa kwa muda mrefu bila hatima yao kujulikana.

“Baba yetu hali yake si nzuri, akimfikiria mwanawe huko aliko. Amekopa fedha kumsaidia, lakini wapi; juhudi zimefanyika lakini hazijawa na tija mpaka sasa, tunaiomba Serikali isikie kilio chetu na itusaidie,” alieleza.

Aliongeza: “Serikali ilifuatilie suala hili limalizike, kwani hakuna linaloshindikana juu ya Serikali. Rais Samia anaweza kulimaliza, walimalize ili anayestahiki basi achukuliwe hatua.

“Tunaiomba Serikali sisi ndio wenye ndugu, wako huko, tumekwenda sana mahabusu, kila siku miguu haiishi kwenda kuwaangalia hadi uchungu, kibaya zaidi wengine familia zao zimeharibika sana tangu walipokamatwa,” alisewma.

Mbali na mashekhe hao 186 wanaosota rumande kwa tuhuma za ugaidi, inadaiwa kuna wengine wako mahabusu za mikoa mbalimbali, wakiwamo 61 walio Arusha, Mwanza (52), Geita (14), Morogoro (21) na Mtwara (25).
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad