Illustration of William Gallagher
Kwa wasikilizaji wake , William Neil "Doc" Gallagher alifahamika kama daktari wa pesa "Money Doctor" - mtu mwenye pesa ambaye alitangaza huduma zake kwenye radio ya Kikristo , iliyotangaza kote nchini Marekani kutoka kile kilichoitwa ukanda wa Biblia- 'Bible Belt' eneo lote la North Texas.
Matangazo yake ya biashara mara kwa mara yalikamilishwa kwa usemi uliokuwa maarufu kwa wengi: "Tukunane kanisani Jumapili ."
"Dokta Neil Gallagher ni Mmarekani halisi, mwenye haiba katika mambo yote anayoyapenda,", alisema msimulizi katika video ya kampuni ya Gallagher iliyotumwa kwenye mtandao wa YouTube. "Mwenye ari ya kuwasaidia watu kustaafu salama, mapema na wenye furaha .", alisema msimulizi huyo wa video yake iliyomtangaza.
Watu 20 wafariki wakikimbilia mafuta ya upako Tanzania
'Nabii' aliyeshindwa kumfufua mfu akamatwa Ethiopia
Taarifa usizozijua kumhusu Nabii Bushiri na mkewe
Video hiyo ya dakika tatu inaendelea kusifia faida za kuwa mfuasi wa Bw Gallagher ikielezea kuwa ni mtu mwenye "mtindo wa maono ", kwa madai kuwa ameweza kuwaelekeza zaidi ya watu 1,000 kujitegemea kifedha kupitia kampuni yake inayoitwa, Gallagher Financial Group, huku pia akichapisha kitabu kinachoitwa Yesu Kristo, Bwana wa pesa- , "Jesus Christ, Money Master".
Hata hivyo kwa hali halisi, Bw Gallagher hakuwa na lolote la maana , bali alikuwa tapeli aliyeiba dola milioni 32 (£24m) katika mpango ulioitwa Ponzi ambao zaidi uliwalenga waathiriwa wastaafu wenye umri wa kati ya miaka 61 na 91.
Katika mfumo wa Ponzi, wawekezaji wa mwanzo walipata "faida" kwa kuchukua pesa kutoka kwa wawekezaji waliowekeza baadaye, ambao mara kwa mara waliahidiwa kupata faida na uwezekano wa kupata hasara kidogo.
Mifumo hii hutegemea kuendelea kujiunga kwa watu wapya wanaotoa pesa kwa wale ambao tayari wamewekeza ili uweze kuendelea. Wakati hilo linaposhindikana, mfumo huo huporomoka.
Kulingana na nyaraka za mahakama, Gallagher alikuwa akitapeli watu kupitia mfumo wa Ponzi tangu mwaka 2013.
Kampuni zake mbili, Gallagher Financial Group, Inc. na W. Neil Gallagher, Ph.D. Agency, Inc. ziliamrishwa na mashirika ya usalama pamoja na tume ya ubadilishaji wa pesa kufungwa mwezi Machi 2019.
Mwezi uliopita Gallagher alipewa hukumu tatu za maisha gerezani zilizotolewa na jaji wa Texas - kaunti ya Tarrant.
Hukumu hizo zimefuatia hukumu ya kifungo cha miaka 25 jela ambayo alikuwa tayari amehukumiwa katika jimbo la Dallas Machi 2020.
Gallagher aliwaahidi waathiriwa wa wizi wake faida ya kati ya 5% hadi 8% ya pesa zao walizowekeza kila mwaka. Badala yake hawakupokea chochote. Huku Gallagher akitumia fedha nyingi kwa matumizi yake na kugharamia matumizi katika kampuni yake na kuwalipa wawekezaji wa awali.
Alificha wizi huu, alitoa pia taarifa feki za akaunti zilizoonyesha kuwa ana pesa kwenye akaunti hiyo , jambo ambalo halikuwa halisi.
BBC haikuweza kumpata wakili wa Gallagher ilipotaka kupata kauli yake.
Badala yake , waathiriwa karibu 200 wa wizi wa Gallagher walionyesha wizi uliokuwa wa aina tofauti: Wizi uliowalenga wakongwe, uhalifu ambao shirika la ujasusi la Marekani FBI linaamini unaongezeka, ukigharimu mabilioni ya dola kila mwaka.
Miongoni mwa watu ambao Gallagher aliwaonea zaidi katika wizi wake walikuwa ni wanawake wenye umri wa miaka 70 na ushee wanaougua magonjwa ya saratani inayoathiri mfumo wa seli nyeupe au lymphoma ambao waliwekeza zaidi ya dola nusu milioni, kwenye mashine za kusindika mchanga za kibiashara, pamoja na wawekezaji , polisi wastaafu wa maeneo mbali mbali.
Waathiriwa wengi walilazimishwa kuuza nyumba zao, kuchukua mikopo kutoka kwa watoto wao au kurejea makazini baada ya kustaafu kutokana na wizi wa Bw Gallagher.
Ilikuwa ni kisa kibaya zaidi cha wizi cha mwanamke mkongwe ambacho hajawahi kukishuhudia maishani mwake ,Lori Varnell, Mkuu wa polisi wa Kaunti ya Tarran, alisema Mwanasheria mkuu wa Wilaya ambaye anasimamia timu ya mawakili watetezi katika kesi ya wizi wa fedha alipozungumza na BBC.
"Hawa ni watu binafsi ambao walifanya kazi maisha yao yote ili kuweka akiba ya pesa zao. Lilikuwa ni jambo la kibinafsi ," Bi Varnell alisema. "Wameumizwa . Haikuwa tu kukosa pesa. Ilikuwa ni usaliti."
Kuwapata waathiriwa hawa, Gallagher alitangaza huduma za kampuni yake katika makanisa na kupitia redio ya Kikristo, ambayo ilikuwa mwavuli uliojumuisha maelfu ya vituo vya redio kote nchini vilivyotangaza vipindi vya Kikristo, kuanzia mahubiri na mazungumzo hadi muziki na taarifa za habari.
Gallagher aligundua kuwa amejenga Imani kwa waathiriwa wake na kwamba hawawezi ''kugundua mengi katika maelezo anayoyatoa " kuhusu kile kilichokuwa kinaendelea'' , anasema Bi Varnell.
Wizi huu wa aina hii umekuwa ukifanyika nchini Marekani. Mwendesha mashitaka Fleck aliiambia BBC kuwa anakumbuka tukio moja mbapo alimshitaki mwanaume mmoja ambaye alikuwa mfuasi wa makanisa sita. Baada ya kuaminiwa na wafuasi, mwanaume huyo aliiba vitambulisho vya watu 25 tofauti aliokutana nao kanisani, akanunua nyumba kwa majina yao , halafu akaanza kupokea pesa za kodi za nyumba kutoka kwa wapangaji.
Katika mfano mwingine, mwanaume mmoja mkazi wa California alikamatwa mwaka 2017 kwa kuwaibia wahamiaji 200 kutoka Armenia kiasi cha dola milioni 19 kwa kuwaahidi kuwekeza pesa zao katika hisa za kiteknolojia zenye faida kubwa.
Maafisa wanasema kwamba wakongwe huwa ndio kundi linalolengwa zaidi na kuathiriwa na utapeli wa aina hii.
Kulingana na FBI, mamilioni ya wazee Wamarekani huathiriwa na utapeli kila mwaka, na hupoteza kwa ujumla zaidi ya dola bilioni 3 kila mwaka.
Jeffrey Cramer, mwendesha mashitaka wa zamani wa serikali ya kijimbo, alisema kuwa wakongwe mara nyingi hulengwa sana na matapeli ambao huamini kuwa wameweka kiasi kikubwa cha akiba.
"Kwa sehemu moja, wana pesa zaidi kwasababu wamekuwa wakifanya kazi kwa muda mrefu.
Mtu mwenye miaka 60 na ushee au 70 na ushee huenda amewekeza katika maeneo mengi na nyumba yenye thamani mara tano ya fedha alizoinunua."
Illustration of William Gallagher's book "Jesus Christ, Money Master"
Lakini aina hizi za utapeli haziwezi kuisha , anasema Bi Varnell. "Mashambulizi ya pamoja " ya matapeli- wengi wao kutoka nje ya nchi yamekuwa yakiiba fedha za wastaafu wa Marekani kwa kiwango cha "mamilioni kila siku", alisema.
Wakongwe na familia zao wanapaswa kuwa macho kung'amua dalili za utapeli.
"Kama wewe ni Mkristo, na mtu fulani anawasiliana na wewe kupitia njia za Ukristo, unapaswa kuwa mwenye mashaka sana ," alisema. "Vilevile usiache kumshuku mtu yeyote kama wewe ni Muyahudi, au Muislam, au mtu . Kama mtu akiwasiliana nawe kwa misngi ya kidini, unapaswa kuwa mwenye mashaka sana."