Licha ya kwamba inatokea mara chache sana kwa mwanamke kupata mimba mbili kwa wakati mmoja, au kupata ujauzito akiwa mjamzito, wataalamu wanaorodhesha sababu tatu za kibaiolojia ambazo zinapelekea ugumu wa hilo kutokea.
Kwa mujibu wa mtandao wa healthline.com kuna vitu vitatu vinatokea kwenye mwili wa mwanamke akipata ujauzito, vitu vinavyozuia mwanamke huyo kupata ujauzito mwingine katika kipindi cha miezi tisa.
Mosi, mayai kutozalishwa ama kutoka. Kawaida mwanamke anahitaji kutoa yai lenye afya ili apate ujauzito. Mara baada ya yai la kwanza kutoka na kufanikiwa kurutubishwa na kupandikizwa kwenye mji wa uzazi, homoni za uzazi ama ujauzito hutoa taarifa kwa ovari kwamba mayai hayaitajiki tena kwa sasa. Ikiwa mwanamke ana ujamzito, mji wa mimba hautapokea mayai tena, na virutubisho vyote vitakavyozalisha vitamwambia asijiandae kwa kuzaa.
Jambo la pili, ukizungumzia mji wa uzazi ama mfuko wa uzazi, inakuwa ngumu kwa yai lingine lililorutubishwa ikiwa kuna la kwanza limerutubishwa na kupandikizwa kwenye mji huo.Kawaida utando wa mji huo hutanuka kusaidia kulishika yai la kwanza, hivyo ni ngumu kwa yai la pili kusaidika kwenye kingo za uzazi na utando huu.
Jambo la tatu, wakati wa ujauzito, kuna kitu kinachoitwa 'mucus plug', ni uteute kama makamasi unaotoka kwenye mfumo wa uzazi , ambao kazi yake sio kulinda tu mji wa uzazi dhidi ya maambukizi lakini pia inazuia mbegu za kiume kupita.
Kwa sababu hizi, wataalama wanaendelea kujiuliza inawezekanaje?
Inawezekanaje kupata mimba ukiwa na mimba?
Inawezekana ikawa ni jambo la kushangaza na lisilowezekana katika hali ya kawaida. Lakini inawezekana kwa mwanamke kupata ujauzito mwingine akiwa mjamzito.
Ingawa ni nadra kutokea lakini inatokea na kitendo hicho kitaalamu kinaitwa superfetation"
Kwa maneno mengine na kwa lugha nyepesi iliyozoelekwa waweza kusema mwanamke huyu, amepata mimba ya watoto mapacha, lakini watakuwa katika namna tofauti na muda tofauti, na mara nyingi watazaliwa tofauti kabisa sio kwa kufatana kwa muda mfupi kama mapacha wa kawaida ilivyozoeleka.
Mwanamke mwenye mimba mbili huwa na watoto tumboni wanaotofautina kwa vitu vingi ikiwemo kimo na damu.
Ingawa kuna tofauti kati ya kurutubishwa kwa yai lililorutubishwa tayari au kupandikizwa kwa kijusi cha kike. Urutubishaji wa mbegu za kiume ndani ya mayai mawili kwa wakati mmoja kupitia kitendo kinachoitwa kitalamu 'superfecundation', basi mwanamke huyu atazaa mapacha.
Ikitokea mayai mawili tofauti yakarutubishwa kwa mbegu za wanaume wawili tofauti ndani ya saa 24 katika mzunguko huo huo mmoja wa hedhi, mwanamke huyo anaweza kupata ujauzito wa watoto wenye baba wawili tofauti.
Lakini katika kile tunachozungumzia mwanamke kupata ujauzito ama mimba nyingine akiwa mjamzito tayari, maana yake ana mimba mbili , na kila mtoto wakati wa ujauzito huu wa pili, watakuwa na viwango tofauti vya makuzi yao tumboni, watakuwa na damu tofauti, na huenda wakatofautiana kabisa vitu vingi.
Visa vya wanawake waliopata mimba mbili duniani
Mpaka sasa kuna visa kama 10 vilivyoripotiwa duniani kuhusu wanawake waliopata ujauzito wakiwa wajawazito, ingawa inaelezwa huenda kukawa na visa vingi tu ambavyo hajiweza kurekodiwa. . Hivi karibuni huko nchini Australia mwanamke anayeitwa Kate Hill, ambaye amekuwa na aina hii ya ujauzito mara mbili kwa siku 10.
Alijaliwa kuwa na mabinti wawili, Charlotte na Olivia, ambao waliitwa mapacha, ingawa walikuwa na siku kumi tu za kuishi.
Wote walizaliwa siku moja, lakini walikuwa na kimo tofauti na aina ya damu tofauti.
Ni jambo linaloshangaza wengi, lakini hutokea kwa nadra, mwanamke kupata mimba mbili kwa wakati mmoja
Kibaiolojia, suala hili kama halipaswi kutokea, kawaida vichocheo ama homoni za mimba huzuia ama hufunga mfumo wa mwanamke, na kumfanya ashindwe kutoa mayai wakati wa ujauzito. 'Ndio maana ujauzito juu ya ujauzito ni jambo la kushangaza', anasema Connie Hedmark kutoka Hospitali ya Michigan kama alivyonukuliwa na mtandao wa Babycenter.
Hakuna anayejua hasa kwa hakika, kwanini hili linatokea, lakini kwa mujibu wa Karen Boyle, mtaalam wa tiba za uzasi, ujauzito juu ya ujauzito inaweza kutokea pale ambapo upandikizaji wa kiini tete cha kwanza kinapochelewa, kinazuia kuchochewa kwa homoni kupanda viwango.
Na kuchelewa huku kwa upandikizaji kunaelezwa kutokea zaidi kwa panya na baadhi ya wanyama (ingawa hili halijafitiwa sana, kwa mujibu wa mtandao wa babycenter).
Wanyama huzaa mapacha na hii ni kawaida kabisa kutokewa kwa panya, sungura, na kondoo, na pia samaki na wanyama wengine