Faru wa Tanzania Ruksa Kuoa Kenya



Wakati Tanzania ikiipatia Kenya ndege aina ya Korongo 20 kama zawadi ya Krisimasi, Kenya imekubali Faru wa Tanzania waoe Kenya.

Ndege 20 waliotolewa kwa Kenya kutaifanya nchi hiyo kuwa na ndege hao 32 kutoka 12 waliopo sasa kwani Tanzania ilikuwa nao 4000.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Desemba 10, 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan wakati akifafanua baadhi ya maeneo ambayo yamewekewa makubaliano kati ya nchi hizo mbili ikiwemo utalii, nishati, ulinzi wa mipaka na sekta ya afya.

Katika sekta ya utalii, Samia amesema ikolojia ya Tanzania na Kenya ni moja ila imegawanywa na mipaka huku akibainisha kuwa wamewataka mawaziri wa eneo hilo kukaa, kuzungumza na kuondosha changamoto ili nchi zifaidike kuleta watalii wengi na kupata mapato.

Amesema sekta hiyo kwa upande wa Kenya walikuwa wakiona ndege korongo wakiwa Tanzania na wakati mwingine katika kutembeza watalii walikuwa wakiwaulizia lakini hawapo nchini kwao hivyo ilibidi watalii watembee kuja Tanzania

“Hivyo nina furaha ya kumkabidhi cheti cha ndege korongo 20 Rais Uhuru Kenyatta ambao watapelekwa Kenya ili wakae katika mbuga zao. Na watafika kabla ya kristimas kama zawadi ya sikukuu kutoka Tanzania,” amesema Samia.

“Lakini namimi nikatumia fursa hapohapo kumwambia (Rais Uhuru) katika mbuga zangu kule Ngorongoro huenda na Serengeti nina madume tu mafaru wawili hawana wenza nikamwambia siyo vibaya wakioa Kenya, sisi tuko tayari kutoa mahari tupate mafaru majike kutoka Kenya waolewe Tanzania,”

Samia amesema Rais Uhuru alikubaliana na ombi hilo na kuongeza kuwa siku ya kuwapokea lazima keki ikatwe ya kusherehekea ndoa ya mafaru.

Katika upande wa ushirikiano wa Sekta ya afya amesema wameagiza kuwepo ushirikiano katika mapambano dhidi ya Uviko 19.

“Tumewaagiza mawaziri, washirikiane, walifanyie kazi kwa sababu nchi zote ni wahanga wa ugonjwa huu. Sote tumepokea maradhi haya lakini sote pia tunafungiwa na kunyimwa haki wakati mwingine ya kutembea kwenda nje au watu kuwekewa mipaka kuja kwetu kutokana na maradhi haya,”

“Hivyo tumekubaliana tushirikiane katika kupambana na adui huyu,”

Katika uimarishaji wa mipaka ya nchi amesema pia limezungumzwa vizuri na kazi hiyo imeachwa kwa mawaziri wahusika

Katika upande wa bomba la gesi kutoka Tanzania kwenda Kenya pia limeachwa kwa mawaziri wa nishati walishughulikia kwa sababu wale wa upande wa Mombasa wanapata steamer yao kwa kutumia mafuta

“Wenzetu Kenya Mungu hawakuwabariki gesi sisi tunayo hivyo tutalaza bomba kutoka Tanzania hadi Mombasa ili ikazalishe steamer na gesi ya kupikia nyumbani. Hili tumewaachiwa mawaziri wamalize halafu ngazi za juu tutakuja kumalizia ili mradi uanze,”

Amesema mikataba hiyo imetokana na vikao vya tume za ushirikiano ambapo Agosti mwaka huu walikutana na kufanyia kazi mambo mengi.

Alitumia nafasi hiyo kuwaambiwa mawaziri wa Kenya na Tanzania kuwa hiyo ndiyo njia ambayo wanapaswa kwenda nayo ili nchi hizo zinawiri na mataofa hayo yawe na sauti na nguvu za kiuchumi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad