Fei Toto fundi anayewaumiza vichwa Msimbazi




SALUTI kwa jicho lililoona kipaji cha kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’, mzaliwa wa Zanzibar kwani tangu ajiunge na wababe hao wa Jangwani 2018 huduma yake imeendelea kuwa muhimu.

Makocha waliopita ndani ya klabu hiyo tangu 2018 - 2021 hawakuacha kumtumia Fei Toto (23) kwenye vikosi vya kwanza, jambo linalodhihirisha ubora wa kipaji chake.

Kwa kile ambacho amekuwa akikifanya Fei Toto, Simba wanapaswa kuwa naye makini leo kwenye dabi maana ni kati ya wachezaji wa Yanga ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi kinachonolewa na Nasreddine Nabi.

Katika mechi saba ilizocheza Yanga imeshinda sita na sare moja dhidi ya Namungo na inamiliki pointi 19 na mabao 12, ambapo kati ya hayo idadi kubwa imechangiwa na fundi huyo.


 
Fei Toto amechangia mabao matatu dhidi ya Kagera Sugar (dk 24), KMC alitoa asisti ya bao la Fiston Mayele (dk 5) na alifunga (dk11), Ruvu Shooting alifunga (dk 32) na Mbeya kwanza alitoa asisti ya bao la Mayele na kusababisha faulo ya bao la Said Ntibazonkiza ‘Saido’.

BADRU AMCHAMBUA

Kutokana na ubora wa Fei Toto aliyekuwa kocha wa Gwambina na Mtibwa Sugar, Mohammed Badru alimzungumzia Fei anavyoweza kuwa mwiba kwa Simba.

Badru ambaye ni kocha wa timu za vijana za Azam, anasema kama kiungo huyo atacheza kwenye kiwango chake ni wazi kuwa Simba watakuwa na wakati mgumu kutokana na uwezo wake wa kuchezesha timu na kupachika mabao ambao ameuonyesha kwenye ligi.


“Tumeona Fei akifunga na kutengeneza nafasi. Kwangu ni mchezaji hatari zaidi kwa Yanga kwa sababu ana uwezo wa kuutafuta mpira ukipotea, anaweza kutengeneza nafasi na kuzitumia. Kama atakuwa sawasawa inaweza kuwa faida kwa timu yake,” anasema kocha huyo.

PLUIJM ATOA NENO

Aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans van Pluijm anasema kwa mara ya kwanza aliona kipaji cha Fei Toto 2017 wakati timu hiyo ilipokuwa ikishiriki michuano ya Mapinduzi visiwani Zanzibar, kisha akamwambia meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh awaambie viongozi wamsajili fasta.

“Japokuwa tulipishana, niliondoka 2017 aliingia 2018, kile ambacho nilikiona kwake naendelea kukishuhudia, kwani namfuatilia sana. Ana kipaji ki-kubwa na anaweza akacheza nchi yoyote kwa Afrika,” anasema.

Naye kocha msaidizi wa timu hiyo, Cedrick Kaze aliwahi kumzungumzia Fei Toto kwamba ni mchezaji anayeweza kumudu nafasi ya kiungo mkabaji na mshambuliaji.


 
“Kipindi tulichokuwa tunamtumia kama kiungo mkabaji palikuwa hakuna mtu wa kufikia uwezo wake. Baada ya kusajili wengine ambao wanacheza vizuri eneo hilo, tumemuweka kiungo ya juu anakofiti zaidi na amekuwa na mchango mkubwa wa mabao,” anasema.

STAILI YA UCHEZAJI

Feisal ni mzuri akiwa na mpira na bila mpira kutokana na sifa mbili tofauti alizonazo.

Kwanza ni mchezaji ambaye anaweza kuwa msaada wakati timu ikiwa haina mpira kwani ni mwepesi wa kukaba, hivyo Yanga itakuwa na faida hiyo ikiwa haina mpira kwenye mchezo dhidi ya Simba.

Jambo lingine ni kwamba ni mzuri kucheza kwa nafasi na amekuwa akijua wapi anapaswa kukaa ili kuwa na madhara zaidi kwa timu pinzani, hivyo mabeki wa Simba watakuwa na kazi kubwa ya kumdhibiti kiungo huyo ambaye bila shaka atacheza nyuma ya Fiston Mayele.

Kama Aishi Manula atajisahau anaweza kushtuka mpira ukiwa nyavuni mwake kwani Feisal ni miongoni mwa wachezaji wazawa wenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao ya mbali hivyo hii

nayo ni faida kwa Yanga kuwa na mchezaji mwenye sifa hiyo.

Feisal anaweza kuifanya Yanga kuwa na nguvu maradufu kwenye eneo la kiungo cha kati kwa kuwa anaweza kuwa anashuka chini kukaba na au kusaka mipira mara kwa mara kwa ajili ya kuwaongezea nguvu viungo Khalid Aucho na Yannick Bangala ambao wanatarajiwa kucheza eneo la kiungo cha chini.

Kutokana na aina ya mchezo huo, itarajiwe kwamba atakuwa ni mmoja wa mastaa watakaoteka shoo kwa Mkapa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad