Gari linalodaiwa la Sabaya lapokewa kortini kwa kielelezo




 
Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imepokea gari linalodaiwa ni la aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ikiwa ni kielelezo katika kesi inayomkabili.

Sabaya na wenzake sita wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi mahakamani hapo.

Kutokana na aina ya kielelezo hicho, jana Mahakama ilihamia nje ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kulitambua gari lililotolewa kielelezo katika kesi hiyo.

Shahidi wa 12 wa Jamhuri, Sabri Sharif (36) aliiomba Mahakama ipokee gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 222 BDY, akidai kuwa, alimuuzia Sabaya kwa Sh60 milioni.


 
Sharif alikuwa akitoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka.

Ombi la shahidi huyo halikupingwa na mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Mosses Mahuna. Baada ya shahidi kuomba gari lipokewe, Wakili Kweka aliiomba Mahakama ihamie nje lilipokuwa gari hilo.

“Mheshimiwa hakimu, shahidi ametolea maelezo na kielelezo kiko nje ya Mahakama, ili maombi ya shahidi yawe sahihi lazima aweze kutambua kitu hicho. Kwa ridhaa ya Mahakama yako, kielelezo kiko nje, nitaomba Mahakama iende pale ili shahidi akitambue na kuleta ombi lake rasmi,” aliomba Kweka.

Baada ya ombi hilo, Mahakama ilihamia nje na shahidi alilitambua gari hilo kupitia namba za usajili na rangi. Gari hilo lilifunguliwa mlango wa nyuma na ndani kulikuwa na nguo na viatu.

View this post on Instagram
A post shared by Mwananchi (@mwananchi_official)

Baada ya Mahakama kulipokea, shauri hilo liliendelea katika chumba cha wazi mahakamani.

Awali, shahidi huyo alidai kuwa gari hilo analitambua kwa kuwa alikaa nalo si chini ya miezi mitatu.


 
Akimhoji shahidi huyo, Wakili Mahuna alisema: Hii gari unayosema ulimuuzia Sabaya, lini ilikuwa ya kwako?

Shahidi: Mwaka jana kuanzia mwezi wa tisa.

Wakili: Una kadi ya hii gari inayosoma jina lako?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Hii gari uliinunua kwa nani?

Shahidi: Oilcom.

Wakili: Ulinunua shilingi ngapi?

Shahidi: Sh60 milioni.

Wakili: Hapa mahakamani umeleta mkataba wowote wa ununuzi wa gari baina yako wewe na Oilcom?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Kuna wakati wowote baada ya kununua hilo gari uliwahi kuwa na gari inayosoma Sabri Abdallah Sharif?

Shahidi: Nilikuwa na kadi inasoma Oil com.

Wakili: Kuna kipindi chochote gari hii ilikuwa inasoma jina la Philip Haule Njombe?

Shahidi: Hakuna.

Wakili: Kuna mkataba wowote umeleta mahakamani baina yako na Njombe?

Shahidi: Sijaukabidhi bado.

Wakili: Wewe ni muuzaji wa magari.

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Unafahamu usemi unaosema mwenye kadi ndiye mwenye gari, unakubaliana nao?


 
Shahidi: Ndiyo nakubaliana nao kwa masharti.

Wakili: Uliwahi kumtilia shaka Sabaya kuwa hawezi kununua gari la Sh60 milioni?

Shahidi: Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi Wilaya ya Hai unamtiliaje shaka?

Wakili: Ulikuwa na shaka endapo hela hizo ameibiwa Mrosso?

Shahidi: Huko mimi sipo.

Wakili: Ulifahamu hela hizo ni za rushwa?

Shahidi: Siwezi kufahamu.

Wakili: Zilikuwa na harufu ya rushwa kwenye hizo fedha?

Shahidi: Huwezi kujua kama fedha zina harufu ya rushwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad