MBUNGE wa Kuteuliwa Humphrey Polepole ametangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram kwamba hata kata rufaa ikiwa ni Masaa machache tangu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutangaza kuifunga programu yake ya “Shule ya Uongozi” iliyokuwa imerusha episodi 10 tangu ianze.
TCRA ilidai Ijumaa kuwa, Kipindi hicho cha Televisheni cha Mtandaoni cha Mbunge kilikiuka Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui Mtandaoni) za mwaka 2020.
Katika Ukurasa wake ameandika ✍
HATIMAYE HATIMA YA SHULE YA UONGOZI
Ufunuo 2:10b na Ahadi ya 8 ya Mwana CCM visomwe kwa pamoja. Nimetafakari chapchap kwa kina sana. Nimegundua Utume wa Shule ya Uongozi umekamilika na umekamilika kwa Mafanikio Makubwa sana.
Kama zilivyokuwa amri 10 za Mungu kwa Bahati na mimi nilifanikiwa kufundisha na kutoa maarifa katika Episodi 10 ambapo nilijikita katika maeneo tofauti tofauti, kwa 10 hizi zilizosheheni Maarifa, inatosha!
Sitakata rufaa wala sitafanya maboresho katika Shule ya Uongozi kwasababu Utume ukikamilika, Umekamilika hakika! Kwaheri Shule ya Uongozi, nimegundua sisi Viongozi tumetosheka kimaarifa, tunajua, tunafahamu na huwa hatupendezwi na Maarifa ya ziada.
Najua wananchi wa kawaida sana walifuatilia kwa wingi kutoka Mikoa yote na wengine nje ya Nchi. Kwenu wafuatiliaji zaidi ya Milioni 5 wa kawaida Msifadhaike wala Msitahayari bado nina deni kubwa kwenu, nitaendelea kulilipa kwenu kivingine.
Msikate tamaa! Si wahenga walisema safari moja huanzisha nyingine ? Kuhusu kusema kweli, jambo moja nawaeleza hakika Aluta Continua! NB: Kazi ya kufukiza moshi inaendelea