Wakati fulani Wachaga walinasibishwa na Uyahudi. Ilidaiwa kuwa
kabila hilo lina nasaba na Wayahudi wa Ethiopia.
Hata hivyo, kabila hilo linalopatikana kaskazini mwa Tanzania, linaelezwa kuwa limetokana na mchanganyiko wa wahamaji kutoka makabila mbalimmbali wakiwamo Wakamba, Wataita, Wamasai na Wasambaa.
Miongoni mwa waliofanya utafiti na kuandika kuhusu hili ni aliyekuwa mhadhiri wa historia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Isaria Kimambo.
Hao wanaotajwa kama Wayahudi wa Ethiopia wanajulikana kama ‘Beta’ na waliishi katika ufalme uliojulikana kama Aksumite.
Huo ulikuwa ni ufalme wa zamani ambao uliokuwapo katika maeneo ambayo sasa ni Eritrea, kaskazini mwa Ethiopia, sehemu kubwa ya mashariki mwa Sudan na kusini/mashariki mwa Yemen.
Wengine wanawaita ‘Falasha’ au ‘Mafalasha’. Hao hawakuwahi kuhama kuelekea kusini kiasi cha kufikiriwa kuwa ndio waliokuja kulowea kuuzunguka Mlima Kilimanjaro.
Hata hivyo, historia ya ‘Mafalasha’ na ile ya ‘Wachaga’ zinatofautiana sana, kiasi kwamba hakuna mahali popote unapoweza kukuta mfanano wao wowote hata kwenye tamaduni zao.
Hadi mwaka 1975 Mafalasha wengi hawakutambuliwa rasmi kama Wayahudi, na wengi wao walisafirishwa kwa ndege kupelekwa Israeli kati ya mwaka 1984 na 1985.
Kuanzia Alhamisi ya Novemba 21, 1984, Mafalasha takriban 8,000 kutoka Ethiopia walikwenda Israeli. Falasha wa mwisho alisafirishwa Jumamosi ya Januari 5, 1985. Kwa wiki hizo saba, zaidi ya ndege 30 zilishiriki kuwasafirisha Wayahudi hao wa Ethiopia kuwapeleka Israeli.
Ni kweli, kwa mujibu wa simulizi fulani, Malkia wa Sheba (wa Ethiopia) alikutana na Mfalme Sulemani na kuzaa mtoto aliyeitwa Menelik (alikuja kuwa mfalme wa Ethiopia) na kwamba uzao wa Mafalasha hao ulitokana na Menelik.
Lakini kuna uhusiano mdogo au hakuna uhusiano wowote kati ya Menelik na Mafalasha. Kwa wasomaji wa historia, neno ‘Falasha’ linatokana na lugha ya Kiamhari (Amharic) ya Ethiopia likimaanisha ni “watu wasio na makazi” au “watu wa kutangatanga”. Lakini hata kama linahusiana na Menelik, halihusiani na Wachagga.
Kuna madai mengine yasiyo na uhakika wa kihistoria yanayodai kuwa Wachagga ni Waromo waliofukuzwa na Wakamba wakakimbilia kwenye mteremko wa Mlima Kilimanjaro. Kwa hiyo Waromo wanahusishwa na Wachagga au Wachagga wenyewe ndio Waromo.
Simulizi za wanahistoria
Hata hivyo, simulizi za wanahistoria zina jambo tofauti na madai haya. Kwa mfano, Nina Fitzgerald aliyeandika kitabu ‘Somalia: Issues, History, and Bibliography’ na Mohammed Hassen, mwandishi wa kitabu ‘The Oromo and the Christian Kingdom of Ethiopia: 1300-1700’, wanawaleza Waromo kuwa ni kabila la Wakushi (Cushite) na taifa linalopatikana katika eneo la Oromia la Ethiopia na Kenya ambao huzungumza lugha ya Kioromo.
Ni kabila la pili kwa ukubwa nchini Ethiopia. Hawana historia iliyoandikwa ambayo inakwenda nyuma ya karne ya 16. Kwa hiyo ni vigumu kuwahusisha hawa na ‘Mafalasha’ wanaodaiwa kuwako kabla ya Mtume Yesu.
Kuna historia inadai kuwa hawa Waromo walifurushwa tena na Wakamba. Lakini hakuna uhakika wowote wa kihistoria unaotetea madai haya. Historia iliyoandikwa inasema baadhi ya Wachagga walitokana na Wakamba na si kwamba ni kabila tofauti na la Wakamba ambalo ‘lilifurushwa’ na kuhamia Mlima Kilimanjaro.
Yako madai mengine yanasema waliofurushwa (Wachaga) walikimbilia Mlima Killimanjaro na hapo wakawakuta watu wafupi walioitwa ‘Wambuti au Mbilikimo’. Madai haya nayo hayana uhakika wa kihistoria.
Wambuti hawakuwahi kamwe kuishi eneo lolote linalozunguka Mlima Kilimanjaro wala eneo lolote la Tanganyika. Hao wanajulikana kama ‘Bambuti’ ingawa lahaja iliwabadili jina wakaitwa ‘Wambuti’.
Hawa asili yao ni nchi za Afrika ya Kati, hususan Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Maana ya neno hilo ni ‘Watu wa Mwituni’. Kwa hiyo si kwamba walipigwa, wakaondoka, wakaelekea Kongo, bali wao ni wa hukohuko Kongo.
Mfanano wa maneno ya Kichaga na Kiyahudi
Wanaojitahidi kuonyesha kuwa Wachagga wanahusiana na Wayahudi wanaweka maneno ya Kichagga na kuyalinganisha na ya Kiebrania ili kuhalalisha mfanano na uhusiano wake. Neno ‘YAVE’ ni la Kichagga ambalo ni sawa na ‘Yahwe’ la Kiebrania.
Hata kama ‘Yave’ (au Yawe) ni la Kichagga, inawezekana huu ulikuwa ni utohoaji tu. Ni kama neon ‘darasa’ linatokana na neno la Kiarabu; ‘darsa’, na kwa maana hiyo hatuwezi kusema Waswahili ni Waarabu au asili yao ni Waarabu.
Neno jingine ni ‘Eli’ ambalo linawakilisha jina la Mungu, lakini lilichukuliwa kwenye Biblia. Lakini hili nalo halidokezi chochote kuwa Wachagga asili yao ni Wayahudi.
Zinatajwa pia tabia za Wachagga. Lakini hizo nazo hazidokezi chochote kwamba asili ya Wachagga ni Wayahudi. Ingawa zinatajwa tabia nyingi, hapa nagusia moja tu inayodaiwa kuwa Wachagga hawapendi kudhulumiwa au kuonewa kwa namna yoyote ile.
Hata hivyo, hiyo si tabia ya Wachagga peke yao, na hata kama ingalikuwa hivyo, haileti uhusiano wowote kati ya Wachagga na Wayahudi.