Kaka aeleza kauli ya mwisho kabla dada yake kuuawa



Morogoro. Dennis Mashuwe, kaka wa marehemu Magret Mashuwe aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) ambaye mwili wake uliokotwa, amesema marehemu alimueleza kuwa ataendelea kubaki mkoani humo kusubiri cheti chake baada ya kumaliza masomo.
Magret aliuawa Desemba 14 na mwili wa kutupwa katika mashamba ya chuo hicho na mpaka sasa Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia mwanaume mmoja anayedaiwa kuwa mchumba wake kwa madai ya kuhusika.

Akizungumza leo Desemba 22 katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Denis alisema kuwa baada ya mdogo wake kuhitimu walikuwa wakizungumza mara kwa mara na katika mazungumzo yao hakuwahi kumueleza kama alikuwa na mgomvi.

"Mdogo wangu alikuwa mtu wa watu na alikuwa anapenda ibada na mara ya mwisho nilipoongea na kumuuliza kitu gani kinachoendelea kumuweka Morogoro alisema anasubiri cheti chake," alisema  

Kaka huyo wa marehemu aliliomba jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuchunguza kwa kina kifo cha ndugu yao na yeyote atakayebainika aweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.


 
"Mimi sijui nani amemuua mdogo wangu lakini jeshi la Polisi wanaouwezo na mbinu za kubaini aliyehusika ama waliohusika," alisema Denis.

Akizungumzia taratibu za mazishi mara baada ya kuutoa mwili katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro kaka huyo wa marehemu alisema kuwa wanasafirisha kuelekea wilayani Rombo kata ya Shingatini na wanatarajia kuzika alhamisi ya Desemba 23.

Baadhi ya wanafunzi wa SUA waliofika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya rufaa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho walisema mauaji ya muhitimu huyo yamewapa hofu na taharuki.


"Kwa sasa sisi wanafunzi hasa wa kike tunaishi kwa hofu kutokana na tukio hili,” amesema Rita Mbwambo ambaye ni mwanafunzi wa chuo hicho.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad