Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wanasiasa kutumia vizuri uwepo wa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, kwani lengo kuu ni kuwaletea maendeleo wananchi.
Rais Samia ametoa wito huo leo kwenye Mkutano wa Wadau wa Kujadili Hali ya Demokrasia ya Vyama Vingi Nchini uliofanyika leo Desemba 15, 2021 katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Amesema kuwa na mfumo wa vyama vingi na mawazo mbadala haimanishi kuwepo na vurugu, fujo, kauli zenye ukakasi na vitisho na zenye kuamsha hisia za kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.
''Tuliruhusu mfumo wa vyama vingi kwa nia kuruhusu uwepo wa ushindani wa fikra itikadi na sera ili kuwapa wananchi fursa ya kuchangia mawazo ya namna bora ya kuendesha nchi hii na kuwaletea wananchi maendeleo,'' amesema Rais Samia Suluhu.
Aidha ameongeza kuwa, ''Niwashauri viongozi wa vyama vya siasa tutumie fursa ya kuwepo kwa vyama vingi kuwaonesha wananchi kuwa ni kitu gani cha tofauti tutafanya ili kuwaletea maendeleo. Siasa sio kusema uongo, huko nje kuna msemo unasema ukitaka kusikia uongo nenda kwa wanasiasa, sio kweli siasa sio kusema uongo,''.