MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano Dar es Salaam, imeombwa kuweka kipaza sauti (Spika), nje ya jengo hilo, ili wanachama wa Chadema, wanaoshindwa kuingia ndani ya chumba cha mahakama, wasikilize kesi inayomkabili mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Ombi hilo limetolewa leo Jumatano, tarehe 15 Desemba 2021 na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Wilaya ya Segerea jijini Dar es Salaam, Kitomari Stephen, baada ya Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Magdalena Ntandu, kuwataka watu wanaohudhuria kesi ya Mbowe na wenzake, kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19).
Ikiwemo kukukaa umbali wa mita moja katika mabenchi, kuvaa barakoa na kunawa mikono.
“Muweke spika nje mtu akikaa pale asikie,” amesema Kitomari.
Akijibu ombi hilo, Ntandu amesema suala hilo linashindikana kwa kuwa mahakama hiyo inapakana na Shule ya Sheria, hivyo spika ikiwekwa, italeta kelele na kuondoa utulivu kwa wanafunzi kusoma.
Naibu Msajili huyo amesema, awali waliweka spika nje lakini walilazimika kuondoa kutokana na kuleta usumbufu kwa wanafunzi, hivyo watafanya hivyo pindi watakapopata jengo lao.
“Tuliwahi kuweka mbeleni ikashindikana, tunaondoa utulivu katika chuo, wanafunzi wanashindwa kuelewa hata jenereta letu tuliambiwa tuhamishe tukalileta huku. Hiki kinatufanya tushindwe labda siku tukipata jengo letu tutakuwa na uhuru,” amesema Ntandu.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, ni waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Ling’wenya.
Kesi hiyo yenye mashtaka ya ugaidi, inasikilizwa mfululizo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, ambapo upande wa jamhuri unaendelea kutoa ushahidi wake