Kifo Mhitimu SUA Wazazi Waomba Msaada wa Rais

 


Moshi. Wakati maziko ya mwili wa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Magreth Mashuwe(22) yakifanyika juzi kwenye makaburi ya familia katika kijiji cha Shimbi mkoani Kilimanjaro, wazazi wa marehemu wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassani kuingilia kati hili kufahamu waliofanya mauaji ya binti yao.


Wakizungumza na Mwananchi wazazi walisema wanamuomba kubeba tatizo hilo kama lake ili wale waliohusika na mauaji hayo wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.


Mwili wa mwanafunzi huyo ambaye alihitimu masomo ya sayansi ya mazingira SUA uliokotwa kwenye mashamba ya chuo hicho Desemba 18 mwaka huu, huku tayari Jeshi la Polisi mkoani Morogoro likiwa linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za mauaji hayo.


Mama mzazi wa marehemu, Petronila Temu alilieleza Mwananchi kuwa waliwekeza kwa mtoto huyo na kutumia mali nyingi kuhakikisha anapata elimu iliyo bora, ili baadaye aweze kuisaidia familia yake pamoja na wadogo zake.


Alisema kifo cha mwanawe ni pigo kubwa maishani mwake na ni tukio ambalo hakuwahi kufikiria huku akilaumu kwa nini hakwenda kumchukua mwanawe baada ya kumaliza chuo Novemba.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwanangu Magreth. Aliwaahidi wadogo zake kwamba atawasomesha lakini ndoto zake zimezimwa na wauaji,nimeumia mno. Naiomba Serikali ya mama Samia, ninaiamini wakiamua kufuatilia mauji ya mwanangu wana uwezo wa kuwapata hawa waliohusika na mauaji ya ukatili ya mwanangu.,’’ alisema na kuongeza;

“Nakuomba mama yangu Samia uhakikishe hawa watu wamepatikana tujue ukweli wa mauaji ya mwanangu Magreth. Wamemuua mwanangu niliyekuwa namtegemea anisaidie mimi na kuwasaidia wadogo zake.


Baba mzazi aelezea walivyopata taarifa

Akieleza namna alivyopata taarifa za mwanawe, baba mzazi Liberat Mashuwe alisema: “Niliwekeza sana kwenye elimu ya mwanangu ili aweze kuja kuwa msaada kwa familia na kwa Taifa kwa ujumla. Nakumbuka tarehe 13 mwezi huu tulikuwa na mawasiliano na binti yetu, alinieleza anajiandaa kurudi nyumbani baada ya kumaliza masomo yake, baada ya kupata taarifa mwanangu haonekani tulianza kumtafuta tarehe 13 tukawa hatupati mawasiliano yake kabisa tukashtuka, kwani alikuwa hana tabia ya kufunga simu.


“Tuliwapigia wanafunzi ambao alikuwa anasoma nao maana mama alikuwa na mawasiliano yao wakasema hawampati, tukazidi kushtuka basi tukamwomba kijana wetu aende Morogoro chuoni, ili ajue yuko wapi, kijana alienda na akatafuta baadhi ya ndugu na marafiki zake wakawa wanazunguka kujua ni kitu gani kimetokea.

“Wakaenda polisi kutoa taarifa wakasema kama kutakuwa na kitu chochote watatoa taarifa basi kijana akarudi Dar es Salaam. Baada ya dakika chache nikapata simu kutoka chuoni kwake, wakaniambia kuna mwili wa binti umeokotwa baada ya kufuatilia wakajua ni mwili wa mwanangu, kwa kweli niliumia sana kupata taaarifa hizi.

“Wamemuua binti yangu ambaye nilikuwa namtegemea na kuja kulisaidia Taifa katika mambo ya mazingira. Niliji sacrifice” (kujitoa mhanga) na kutoa mali zangu zote ili nihakikishe mwanangu anasome vizuri na katika masomo yake amekuwa akifanya vizuri, lakini naambulia kuona maiti yake? Ee Mungu nisaidie,’’ aliomboleza.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad