KOCHA Jurgen Klopp amekiri kuwa uvumilivu unahitajika huku Liverpool wakiendelea kufanya mazungumzo ya mkataba mpya na Mohamed Salah.
Mkataba wa sasa wa Salah na 'Wekundu' hao unamalizika Juni 2023 na mustakabali wake umekuwa gumzo kwa muda mrefu.
Mshambulizi huyo mahiri ametangaza kwamba, anataka kubaki Anfield, lakini hakuna makubaliano ambayo yamefikiwa kati ya klabu hiyo na mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri.
Inasemekana kwamba, Salah aliiambia MBC Masr TV kwamba mustakabali wake uko "mikononi mwa wasimamizi na wanapaswa kutatua suala hili".
Klopp Jumatatu alisema kuwa msimamo wa klabu hiyo haujabadilika.
Alisema katika mkutano na waandishi wa habari usiku wa kuamkia mechi ya Ligi ya Mabingwa huko Milan: "Tunajua hasa anachohusu na tunazungumza.
“Kuongeza mkataba na mchezaji wa aina ya Mo si jambo unalofanya pale mnakutana kwa kikombe cha chai mchana na kupata muafaka, hilo ni jambo la kawaida kabisa.
"Kwa kweli hakuna kitu kingine cha kusema juu ya Mo. Anazungumza juu yake wakati anaulizwa juu yake, naweza kusema machache tu kwa sababu mengine yote si ya umma.
"Mambo mengi yanaweza kutokea mtu anapojaribu kufanya hivyo. Mo yuko sawa, niko sawa, nadhani tunachotaka sote kiko wazi na mambo kama haya yanahitaji muda, ndivyo hivyo."