JURGEN Klopp amekubali Liverpool hawawezi kujilaumu kutokana na kipigo kutoka kwa Leicester City na amewaonya wachezaji wake kujifunza kutokana na kiwango kibovu walichoonyesha.
Wekundu hao walipoteza kwa bao 1-0 pale kwenye Uwanja wa King Power Jumanne na walishindwa kupunguza pengo la pointi sita dhidi ya vinara wa Ligi Kuu, Manchester City.
Liverpool ambao wamefunga mara mbili katika kila mechi kati ya 28 kwenye mashindano yote msimu huu, walishuhudia straika wao, Mohamed Salah akikosa penalti na Sadio Mane alipoteza nafasi nzuri ya kufunga.
Mchezaji wa zamani wa Everton, Ademola Lookman alifunga dakika tatu baada ya kuingia uwanjani akitokea benchi na kuwafanya Leicester kushinda mfululizo dhidi ya Liverpool.
Kikosi hicho cha Klopp kilipambana kurudisha bao hilo, lakini Leicester walionekana kuwa makini kulilinda.
"Kwa hakika Leicester walistahili ushindi," alisema Klopp akinukuliwa na Amazon Prime.
"Ulikuwa mchezo mgumu. Hatukuwa kwenye ubora wetu, hata kama tulikuwa na nafasi ya kutosha.
"Kile tulichofanya tukiwa na mpira hakikuwa sawa. Tulicheza mchezo mbaya, hivyo tulistahili kufungwa.
"Maamuzi yetu yalikuwa ya hovyo, pengine tulikosa nafasi na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Tulitakiwa kuwa na nafasi zaidi.
"Nafikiri tulianza vizuri, halafu tukamaliza kwa kucheza vibaya. Kuanzia hapo hatukuwa kwenye ubora wetu.