Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC unatajwa kutangaza Bonasi ya Shilingi Bilioni Moja kuwapa wachezaji wao, endapo watafanikiwa kuifunga Young Africans kesho Jumamosi (Desemba 11).
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu mabosi wa Young Africans watangaze Bonasi ya Shilingi Bilioni Moja kama wakifanikiwa kuwafunga Simba katika Dabi hiyo inayotarajiwa kupigwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Taarifa zimeeleza kuwa Wadhamini wa timu hiyo chini ya mwenyekiti wake, Salim Abdallah ‘Try Again’ kwa kushirikiana na mwekezaji wao Mohammed Dewji ‘Mo’ wametenga kiasi hicho cha fedha ili kufanikisha ushindi.
Mtoa taarifa hizo amesema kuwa, bodi hiyo walifanya kikao cha haraka cha kuweka mikakati ya kuelekea dabi hiyo mara baada ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows uliochezwa Zambia.
Ameongeza kuwa wameweka kiasi hicho cha Bonasi kwa ajili ya kuongeza morali na hali ya kujituma katika mchezo huo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.
“Uongozi unafahamu umuhimu wa mchezo huu dhidi ya Yanga, siyo mwepesi ni mchezo unaovuta hisia za watu wengi ambao unaingia kwenye rekodi, hivyo ni lazima tushinde.
“Kuchukua ubingwa wa ligi pekee haitoshi, kuwafunga ni muhimu, hivyo maandalizi yamekamilika na tupo tayari kwa ajili ya mchezo huo.
“Viongozi wamefanya kikao tayari mara baada ya mchezo wa shirikisho dhidi ya Red Arrows, hivyo akili na nguvu zao wamezielekeza katika Dabi, wametoa ahadi ya Shilingi Bilioni Moja kama Bonasi ya wachezaji kama wakiwafunga Yanga,” amesema mtoa taarifa huyo.
Katika kuelekea mchezo huo, Try Again alisema kuwa: “Gari la Simba hivi sasa limewaka baada ya kuwaondoa Red Arrows, nguvu na akili zetu tunazielekeza katika mchezo ujao wa ligi ambao ni muhimu kwetu kushinda.
Katika kuelekea mchezo huo, Young Africans wataingia uwanjani wakiwa vifua mbele baada ya kuwafunga Simba SC bao 1-0 katika mchezo uliopita wa Ngao ya Jamii, ambalo lilifungwa na Mkongomani, Fiston Mayele.
Chanzo:Championi