Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju
SERIKALI ya Tanzania, imesema mwezi huu wa Desemba 2021, huenda ukawa wa neema, kwa vyombo vya habari vilivyofungiwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Kauli hiyo ilitolewa jana Jumanne, tarehe 7 Desemba 2021, jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, katika kikao kazi cha kuchambua mapendekezo 252, yaliyotolewa na Baraza la Haki la Umoja wa Mataifa (UN), kupitia kikao cha tatu cha tathimini ya mapitio ya hali ya haki za binadamu (UPR), kilichofanyika nchini Uswisi.
Ni baada ya washiriki wa kikao hicho kuilalamikia Serikali kushindwa kutekeleza mapendekezo ya baraza hilo la kuimarisha uhuru wa habari na wa kujieleza, ikiwemo kufungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa kwa makosa mbalimbali.
Mpanju alisema, wizara husika imeshachukua hatua ya kulifanyia kazi suala hilo, kama ilivyoelekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe.
“Kuhusu uhuru wa habari na vyombo vilivyofungiwa, wizara imechukua hatua na Rais Samia ameelekeza kwamba, lazima tulimalize. Najua na nina imani mwezi huu ukawa na neema, tutayamaliza,” alisema Mpanju.
Magazeti ambayo yalifungiwa na kumaliza adhabu zao na ma kusitishiwa leseni za uchapishaji na usambazaji; ni MwanaHALISI, Tanzania Daima, Mawio na Mseto.
Rais Samia aliagiza wizara husika, kuvifunguliwa vyombo vya habari vilivyofungiwa ili vianze kufanya kazi hukua akitaka sheria na taratibu kuzingatiwa.