Makaburi takriban 200 kuhamishwa Vingunguti kupisha athari za mto


Baada ya miaka mitatu tangu baadhi ya makaburi ya Vingunguti, jijini Dar es Salaam kusombwa na maji ya Mto Msimbazi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuja na mpango wa kuyahamisha yaliyosalia kuanzia  Jumatatu.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Mashauri amelithibitisha hilo alipozungumza na mwandishi wa Mwananchi aliyefika eneo la makaburi hayo na kujionea uharibifu uliotokana na athari za mto huo, huku baadhi yake majeneza yakiwa yametokeza juu na mengine nguo za marehemu zikionekana.

Mbali na kuzungumza na mkurugenzi huyo, pia liliwatafuta jamaa na ndugu wa marehemu waliozikwa katika makaburi kusikia maoni yao.

Mkurugenzi alieleza uhamishaji wa makaburi hayo utaanza Jumatatu na kuhusisha makaburi 200 yaliyopo mita 10 kutoka Mto Msimbazi na shughuli hiyo itafanyika kwa siku tatu mfululizo.


 
Mabaki ya miili hiyo yatahamishiwa katika eneo la Mwanagati, Kitunda, alisema.

Hakuna fidia

Katika uhamishaji wa makaburi hayo, Mashauri alisema hakutakuwepo na ulipaji fidia kwa kuwa hakuna mradi wowote unaotakiwa kufanyika katika eneo hilo, isipokuwa ni katika kuhakikisha mabaki ya miili hiyo yanahifadhiwa eneo salama.

“Kisheria, fidia ya kuhamisha makaburi hulipwa kama eneo linatakiwa kupisha mradi, lakini pale Vingunguti hakuna mradi wowote tunaotaka kuufanya kwa sasa, ila tu tumeona tuchukue hatua kutokana na eneo hilo kuwa hatarishi kwa miili ya wapendwa wetu waliolala pale.


“Pia hii si mara ya kwanza kufanya hivyo, kwani mwaka jana pia baada ya mvua kunyesha tuliondoa makaburi mengine nane, yaliyokuwa hatarini na kuyapeleka eneo la Serikali,” alisema.

Kwa upande wake, ofisa afya wa Halmashauri ya Jiji, Reginald Mlay alisema maandalizi yapo vizuri, ikiwamo utengenezaji majeneza ya kuhifadhi mabaki ya miili hiyo, na ununuzi wa sanda.

Pia Mlay aliomba ndugu kuwapa ushirikiano ili shughuli hiyo iweze kutekelezeka kwa urahisi na kwamba kwa upande wao, wana watu wa kutosha katika kufukua makaburi hayo na kwamba watamaliza kwa muda uliopangwa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Butiku yalipo makaburi hayo, Nimzihirwa Mjema alisema kwao ni furaha kuona shughuli hiyo ikitekelezeka kwa kuwa kimekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa mtaa huo.


 
Mjema alisema kubomoka kwa makaburi na majeneza kubebwa na maji ni tatizo lililokuwapo kwa zaidi ya miaka mitatu.

Alisema tatizo hilo limetokana na mchanga unaochotwa katika eneo hilo kwa nia ya kuupanua Mto Msimbazi, ambao umekuwa ukisababisha mafuriko.

“Mto huu kama mnavyojua umekuwa ukisababisha mafuriko kwa miaka mingi, na hatua iliyochukuliwa kuondoa maafa haya ni kuchota mchanga,” alisema.

Alibainisha kuwa mabaki ya miili hiyo sasa yataenda kuzikwa Mwanagati kwa gharama za Serikali na tayari watu 180 wameshajitokeza kujiandikisha kwa ajili ya kukubali hatua hiyo.


“Katika kuwashirikisha, tulifanya mkutano na wananchi miezi miwili iliyopita na kuwaeleza nia hiyo ya Serikali ya kuhamisha makaburi hayo na tuliwaweka wazi kwamba hakutakuwa na fidia, jambo ambalo waliliafiki na sasa kinachofuta ni utekelezaji,” alisema.

Hata hivyo, Mjema alisema kati ya watu waliojiandikisha, watano wameomba kutaka kupewa miili yao wakazike wanapojua wao na kubainisha kwamba gharama za kufanya hivyo watazibeba wenyewe na si Serikali.

Wananchi waafiki

Akizungumza alivyopokea hatua hiyo ya Serikali, Suna Ally alisema ni jambo la kushukuru ukizingatia yeye ambaye alimzika baba yake hapo tangu mwaka 1999, alikuta mwili wake umebaki kiwiliwili na kichwa, huku kuanzia kiunoni hadi miguuni ukiwa kumesombwa na maji.

Mwingine, Alistaliki Bosco alieleza kuwa mwili wa mjomba wake waliuzika hapo mwaka 2009, hivyo kuhamishwa na Serikali ni msaada mkubwa kwa kuwa ingekuwa vigumu kwa ndugu kutokana na uwezo mdogo.

Bosco alisema hatua hiyo ni nzuri kwa sababu si vizuri kumzika binadamu alafu achukuliwe na maji.


 
Kwa upande wake Joyce Mrangu, alisema walikuwa wanaumia kwa namna wanavyopita katika eneo hilo na kuona majeneza yakiwa yananing’nia.

Aliongeza kuwa walikuwa wakiona nguo na sanda walizovikwa marehemu lakini kwa kuwa hawakuwa na uwezo wa nini wafanye, waliishia tu kulalamika, hivyo hatua ambayo Serikali imeichukua ni ya kupongeza.

Athumani Ally, kwa upande wake, alisema mbali na makaburi, changamoto nyingine wanayopata wakazi wa eneo hilo kila mvua zinaponyesha, nyumba zinadondoka na mpaka sasa nyumba zaidi ya 200 zilishabebwa na mafuriko.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Habiba Mdumuka alisema kuna haja ya bonde hilo kujengwa kwa kuwa lilishagharimu maisha ya watu na wameshaliongelea mpaka wamechoka, pamoja na viongozi mbalimbali kufika eneo hilo.

Kuruthumu Ally alisema “Hakuna kitu kinachouma kama ndugu mmezika halafu marehemu anaenda kuishia baharini kwa kusombwa na mafuriko,” alisema.

Peter Nyaburu, aliyeishi kwa miaka 26 eneo hilo, alisema kinacholeta matatizo katika eneo hilo ni mabadiliko ya tabianchi na kueleza kuwa kulikuwa na mti aina ya mkongo uliokuwepo hapo zaidi ya miaka kumi, lakini nao ulibebwa na maji hivyo anaiomba Serikali isiishie tu katika kuhamisha mkaburi, bali na kuharakisha ujenzi wa kingo za mto huo ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad