Makada CCM wamvaa Polepole



ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani Shinyanga, Hamis Mgeja wakiwemo makada wengine, wazee wastaafu wa chama hicho na serikali, wamewataka watanzania kupuuza upotoshaji ulionenezwa kwenye vyombo vya Habari na aliyekuwa Katibu Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole. Anaripoti Paul Kayanda – Shinyanga (endelea)

Kwa mujibu wa Mgeja na viongozi hao wastaafu waliozungumza leo tarehe 9 Disemba, 2021 na vyombo vya habari nyumbani kwake kuhusu maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru, Mgeja amesema kuwa hivi karibuni Polepole alisema Hayati Rais John Magufuli, hakuwamaliza ‘wahuni’.


Kada huyo wa CCM, amesema kuwa ukiangalia mwenendo wa Polepole anayoyazungumza sasa hivi katika vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii, ameamua kuupotosha umma na kuigonganisha Serikali iliyopo madarani inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na watendaji wake.

Juzi alipoulizwa kuhusu mwenendo wa Polepole na hatua ambazo chama kinachukua, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amesema suala la kada huyo na Mbunge wa kuteuliwa na Rais, linahusu vikao vya juu vya chama ambavyo havijaanza kukutana.


 
Hata hivyo, tayari Polepole alishaitwa na Kamati ya Wa bunge wa CCM na kuhojiwa kuhusu mwenendo wake na taarifa inapaswa kuletwa ndani ya vikao vya juu vya maamuzi vyama chama hicho tawala.

“Polepole ni mpotoshaji muungwana kwamba anataka ionekane kwamba kuna tofauti kubwa ya Serikali iliyopita na Serikali iliyopo sasa na kujifanya kuwa yeye ndiye mwana CCM na msema kweli sana, sasa kwa mambo hayo ndugu zangu wazee tusipo yazungumza, huyu mtu tutampa nafasi kubwa ya kuendelea kulipotosha taifa,” aemsema Mgeja.

Amesema kauli za Polepole hasipaswi kuvumiliwa sio tu na viongozi bali pia makada wa chama hicho na ndio maana wao kama viongozi wa zamani, hawamjui Polepole ametoka wapi katika siasa za nchi, hivyo wanatumia fursa hiyo kumuonya na kumtaka akae kimya.


Amesema iwapo Polepole akiendelea kuupotosha umma na kuanza kuwabagua watanzania ili kutengeneza matabaka kwa kauli na lugha isiyo na staha kuwa rais Magufuli hakuwamaliza wahuni, watachukua hatua kubwa zaidi ikiwemo kumshitaki nda ni ya vikao vya chama ili atimuliwe uanachama.

“Ukianza kuwaita wahuni wakati huna vielelezo, huoni kuwa huo ni upotoshaji mkubwa? alihoji Mgeja ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Hamshauri Kuu ya Taifa (NEC).

Kufuatia hali hiyo Mgeja pamoja na viongozi hao, wamewaomba viongozi CCM kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya Polepole ili kukomesha tabia yake na ukosefu wa maadili katika utendaji wake wa kazi.

Raia Mwema lilipomtafuta Polepole kupitia simu yake ya mkononi kuzungumzia hatua ya makada hao kulalamikia, kama kawaida yake hakuweza kupokea licha ya simu yake kuita muda mrefu.


 
Aidha Mgeja akizungumzia kuhusu miaka 60 ya Uhuru alisema, wanaipongeza serikali ya Rais Samia kwamba mpaka sasa katika kutimiza miaka 60 ya Uhuru, mambo yanakwenda vizuri, amani imetawala, na anaendelea kuchapa kazi kwa kasi ile ile ya mtangulizi wake.

Pia alitumia mwanya huo kuipongeza Sekretarieti ya CCM, inayoongozwa na Katibu Changolo kwa kazi nzuri ya kiutendaji na kwamba hawa ndiyo watendaji wanaotokana na CCM kwani hawakuibuka kama Polepole na genge lake.

Pamoja na mambo mengine, Mgeja na jopo la makada hao wa CCM, walitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia kwa kuendeleza utawala bora, kufungua milango ya biashara nje ya nchi pamoja na kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, ukiwemo ujenzi wa vyumba vingi vya madarasa.

Hata hivyo, mmoja wa makada hao, Charles Kishuli, aliikumbusha serikali kuzingatia pindi wanapofanya teuzi mbalimbali za nafasi za uongozi, kuwapeleka watumishi hao vyuo vya serikali kwa lengo la kujifunza maadili ya utumishi wa umma badala ya kuropoka hovyo na kukivua nguo chama.


Kishuli aliongeza kuwa Polepole huenda hakupita chuo cha siasa kwa vile aliibukia kwenye Tume ya Katiba Mpya iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na baadaye akateuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya, kisha akapata nafasi ya kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.

“Kwa kweli PolePole hatendi haki kushambulia viongozi waliomuweka madarakani kwa pamoja sisi kama viongozi wastaafu na makada wa chama hiki tunamuomba aache mara moja vinginevyo chama kichukue hatua ya kumwajibisha,” alisema Charle Kishuli mkuu wa Wilaya Mstaafu na kada wa CCM.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad