Malumbano ya Bulembo, Nape na Polepole kuna msingi umekatika CCM



 
Miaka miwili iliyopita makatibu wakuu wastaafu CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba walitoa waraka wenye kueleza masikitiko yao jinsi ambavyo hawakuwa wakitendewa haki.

Kinana na Makamba walieleza kwamba alikuwepo mtu aliyejiita mwanaharakati, aliwarushia tuhuma nzito kuwa wao walikuwa wakifanya vitendo vya kumhujumu aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli.

Walieleza kushangazwa kwao na ukimya wa viongozi wa CCM, kwamba wakati mwanaharakati huyo akiibua tuhuma nzito, hakukuwa na tamko la chama lenye kuonesha kuingilia kati.

Wastaafu hao walisema kuwa mtu huyo aliyewatuhumu, ilivyoonekana, alikuwa akilindwa na nguvu isiyohojiwa na yeyote. Hiki kilikuwa kipengele nyeti kwa chama kwamba hakikuwa na msingi wa kushughulikia mambo yake ndani kwa ndani.


 
Anatokea mtu, anatuhumu viongozi wastaafu waliokiongoza chama hicho katika ngazi za juu kabisa. Halafu huoni chama kikiingilia kati. Msingi wa nidhamu upo wapi? Kwa nini viongozi wa chama hawakutaka angalau kukutana na wazee ili wazungumze?

Si kuzungumza tu, bali hata kuchunguza ukweli wenyewe. Je, ni kweli Makamba na Kinana walihusika na uhujumu au walisingiziwa? Ukimya wa chama ulidhihirisha aibu kubwa mno kwa taasisi ya CCM ambayo ni kongwe mno.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alitajwa. Badala ya chama kumwita aliyetaja athibitishe tuhuma alizotoa ili na Membe ajitetee, aliyekuwa Katibu Mkuu CCM, Dk Bashiru Ally akaibuka, akasema Membe angehojiwa.


Ni kama Makamba na Kinana, baada ya kutoa waraka wao, badala ya kuitwa ndani wazungumze, likatolewa tamko la Halmashauri Kuu CCM la kuwachukulia hatua. Walicholalamikia kilipuuzwa, wakashughulikiwa.

Hali ileile ya chama kukatikiwa misingi, ipo leo. Hivi sasa kuna malumbano ya wanachama watatu wa CCM, Nape Nnauye, Humphrey Polepole na Abdallah Bulembo.

Polepole alianza kusema kwa kurusha madongo kwamba ndani ya serikali kuna watu wahuni wenye kujali masilahi yao binafsi kuliko taifa. Nape alikuja juu kutaka Polepole ataje majina ya wahuni aliowamaanisha.

Hata hivyo, Polepole hakutaja majina ya aliowaita wahuni na baada ya neno hilo “wahuni” kuibua mjadala, hasa kufuatia hoja ya Nape kwamba wahusika watajwe, Polepole alisema: “Neno wahuni sijaanza nalo leo, wahuni wanaopenda maslahi binafsi kwanza wapo.


 
“Mhuni ni mhuni tu hawabadiliki, nitoe rai kwa viongozi wawe macho na wahuni, awamu jana alitukana Serikali leo anakaa upande wa Serikali.”

Tafsiri ya wengi, maneno ya Polepole kuhusu serikalini kuwepo wahuni ni kipimo cha jinsi asivyokubaliana na mwenendo wa Serikali, ndipo Bulembo alipoibuka, akasema lengo lake si kumjibu Polepole, isipokuwa ni kuweka mambo sawa. Mwisho kabisa akawa amemjibu Polepole.

Hivi karibuni, Nape aliandika fumbo kwenye akaunti yake ya Twitter, akisema: “Aaaah kiroboto, ulishindwa akiwepo godfather, utaweza leo? Kina wenyewe sheikh. Lakini ni kawaida punda roho ikiwa inaacha mwili hurusha mateke. Nonsense!”

Nape hajawa tayari kutaja maana ya ‘twiti’ yake wala mtu aliyemwita kiroboto, ingawa wengi wameipa tafsiri kuwa ni mwendelezo wa mvutano wa Polepole na Nape. Wenye karama ya kutafsiri mafumbo wanafumbua fumbo la Nape kwamba Polepole hakumweza kipindi cha uongozi wa Dk John Magufuli, hatathubutu hivi sasa.


Swali; kwa nini wanachama wa CCM wanalumbana halafu viongozi wanakuwa kimya? Misingi ya chama imepotea? Inakuwaje wahusika wanalumbana kwenye vyombo vya habari halafu hawaitwi ndani ya vikao ili kuzungumza?

Yupo mtu atajibu kuwa huwa wanaitwa lakini si kila wanapoitwa itangazwe. Kuna ambaye atauliza; mbona hivi karibuni Polepole alisema aliitwa na kujieleza? Binafsi swali hilo nilijibu kwa swali; mbona baada ya kuitwa hakuna ukimya na kelele ndio zinazidi?

Tuwe wakweli, kuna mahali msingi wa CCM umepotea, kuna wakati kila mtu anajihisi anajiongoza mwenyewe. Inawezekana vipi kwa chama, tena kinachotawala na chenye historia kubwa barani Afrika, kikose msingi wa uongozi?

Polepole ni mbunge, ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, vilevile ni mwanachama wa kamati ya wabunge wa CCM. Hivyo, analo jukwaa la kutoa dukuduku lake kwa mtindo wa kuwasilisha hoja. Amechagua kutotumia majukwaa yote hayo na kuanzisha kitu anachokiita “Shule ya Uongozi”.

Inawezekana haoni kama yupo huru bungeni wala hajisikii amani kutumia vikao vya chama kutoa dukuduku lake. Je, ni sawa kutoa manung’uniko yenye kupingana na msimamo wa viongozi wa chama nje badala ya kutumia vikao vya ndani?


 
Wapo watu wanaamini kuwa programu ya “Shule ya Uongozi”, ambayo Polepole ameianzisha kupitia intaneti, ni jukwaa la mwanasiasa huyo kutema nyongo dhidi ya yanayoendelea kwenye siasa kwa sasa.

Polepole kwa sasa anawekwa kwenye fungu la watengwa kwenye chama (CCM), sawa na Nape alivyokuwa wakati wa uongozi wa Dk Magufuli. Sauti ya Nape akimteta Dk Magufuli ikadukuliwa, ikavujishwa, ikabidi aende Ikulu, Dar es Salaam, akaombe radhi. Hali ilikuwa mbaya. Je, hadi sasa inaendelea?

Zama za akina January Makamba kudukuliwa akizungumza na baba yake, au Kinana na Nape, ziendelee? CCM wanatakiwa kujifunza kwa yaliyopita. Waishi kama chama. Si kikundi cha misuguano na ubishi wa wenyewe kwa wenyewe kila wakati. Viongozi wa chama hawapaswi kukaa kimya kipindi cha misuguano ya wanachama.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad