Mambo 6 Muhimu Hotuba ya Samia




RAIS Samia Suluhu Hassan amelihutubia taifa, akibainisha mafanikio muhimu sita katika miaka 60 ya uhuru.

Katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia leo, Mkuu wa Nchi huyo alisema Watanzania wana kila sababu ya kutembea kifua mbele kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi hicho cha milongo sita.

Alisema nchi imepiga hatua kubwa kimaendeleo, akibainisha mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kulinda uhuru wa nchi na mipaka yake; kujenga umoja wa kitaifa, amani, utulivu na mshikamano wa wananchi; na kuumairisba uchumi na kupunguza umaskini, akijivunia nchi kuingia katika uchumi kati.

Rais Samia aliyataja mafanikio mengine ni kuongeza upatikanaji na kuboresha huduma kwa wananchi; kujenga heshima ya nchi ushawishi kikanda na kimataifa; na kuimarisha demorasia na utawala wa sheria nchini.

"Ninalipongeza Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa kazi nzuri iliyofanikisha nchi yetu kutopoteza hata kipande kidogo cha ardhi. Jeshi letu lina weledi na kutumainiwa barani Afrika, likishiriki programu za Umoja wa Mataifa (UN) za kutetea amani. Asanteni sana JWTZ," alipongeza.


Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia pia alizungumzia mchango wa ligha Kiswahili katika kuimarisha umoja na mshikamano nchini, akisisitiza kuwa lugha hiyo imekuwa nguzo muhimu katika kuyaunganisha makabila yote zaidi ya 120.

Alisema jambo hilo halikuwa rahisi kwa kuwa wakati nchi inapata uhuru, Kiswahili kilikuwa hakizungumzwi na wengi, lakini sasa Tanzania imefanikisha kushawishi lugha hiyo kutumika katika shughuli za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) huku UNESCO wakitangaza kuwa siku maalum ya lugha ya Kiswahili kila mwaka.

Rais Samia alisema uchumi wa nchi umekua, akikumbusha Tanzania imeingia uchumi wa kati kabla ya mwaka wa malengo (2025) huku wastani wa pato la mwananchi likipanda kutoka Sh. 776 mwaka 1961 hadi Sh. milioni mbili mwaka jana (2020). Pia alisema sekta ya usafirishaji imeimarishwa katika maeneo yote, akitoa mfano kwamba sasa mtu ana uhakika wa kufika mkoa wowote ndani ya saa 24 kwa barabara. "Usafiri wa anga nchini sasa si anasa tena.


Kufufuliwa na kuimarishwa kwa ATCL (Kampuni ya Ndege Tanzania) ni jambo la lazima. Kwa sasa shirika (kampuni) lina ndege 12 na tumekamilisha ununuzi wa ndege zingine tano," alibainisha.

Rais Samia pia alisema kwenye sekta ya nishati kumeshuhudiwa mafanikio makubwa, akibainisha kuwa kukamilika kwa mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere (Mw 2115) kutaimarisha zaidi upatikanaji wa umeme nchini.

Alisema Watanzania wanapawa kujivunia kuboreshwa kwa huduma za wananchi, mfano maji, afya na elimu, akikumbusha kuwa wasomi wa shahada wa kwanza walikuwa 30 tu wakati nchi inapata uhuru na chuo kikuu kilikuwa kimoja tu.

"Sekta ya maji haikuwa na wataalamu, hatukuwa na wataalamu wa Tehama, vyuo vikuu sasa vipo 30, vyuo vikuu 18 ni vya serikali, vyuo vikuu vishiriki vipo 17," alisema.


Rais alikumbusha kuwa zamani waliopata nafasi ya kujiunga na shule za sekondari walikuwa wachache, lakini sasa mamilioni wanakwenda sekondari na kusoma bila kulipa ada. "Shule 1,746 za msingi zinamilikiwa na sekta binafsi. Kabla ya uhuru hazikuwapo. Hospitali za kibingwa ni tano na Hospitali ya Taifa ni moja," alisema.

Rais Samia alisema kuimarishwa kwa huduma za kibingwa kumepunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kupatiwa matibabu hayo.

Alibainisha kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iko mbioni kuanza kutoa huduma za upatikizaji wa mimba. Rais alisema umri wa kuishi wa Mtanzania umepanda hadi wastani wa miaka 67 kwa sasa kutoka wastani wa miaka 37 wakati wa uhuru mwaka 1961.

Hata hivyo, alisema hali ya udumavu nchini bado si nzuri, akiitaka Taasisi ya Chakula na Lishe kuchukua hatua zaidi kukabiliana na baa hilo.


"Kimataifa tunaaminika na Watanzania wanapata nafasi za kuongoza taasisi za kimataifa huku balozi zetu zikiongezeka. Tuna urafiki na nchi nyingi, hatuna nchi ambayo tuna uhasama nayo. "Hata walio na misimamo tofauti na yetu tumewaheshimu huku tukilinda diplomasia yetu. Mafanikio haya yametokana na utawala wa demokrasia na misingi ya sheria.

"Wananchi wamekuwa wakichagua viongozi wanaowataka kuwaongoza. Ndani ya Bunge letu wabunge walikuwa 80 wakati tunapata uhuru lakini sasa wapo 193, waliopo ni 391 -- wanaume ni 248. "Nchi inalinda na kuheshimu haki za binadamu. Vyombo vya habari... vimeendeela kuwa huru na vinaongezeka. Kulikuwa na chombo kimoja tu wakati tunapata uhuru. Mihimili ya dola imeendelea kuheshimiana," alisema.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha amani, utulivu, umoja na mshikamano huk wakitunza mazingira na kuyalinda ili kurithisha vizazi vijavyo.

DIRA YA TAIFA

Rais Samia alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 iko mbioni kufikia ukomo kukiwa na lengo la kuwa na ukuaji wa uchumi wa asilimia nane.

Alisema mkakati uliopo ni kuandaa dira ya miaka 25 ijayo ambayo itajikita kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja kupitia sekta kama kilimo, uvuvi na ufugaji.


"Tuna kila sababu ya kujivunia mafanikio yetu, tulipofika si haba, tutembee kifua mbele, tusijipe unyonge. Tusiangalie kimo, bali kina cha mafanikio tuliyofikia," Rais Samia alihitimisha.

Katika hatua nyingine, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, jana walikuwa miongoni mwa wakuu wa nchi waliotua nchi kwa ajili ya kushiriki kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad