Dar es Salaam. Si jambo rahisi kwa mtu kujivisha ujasiri wa kuua mzazi wake kwa sababu yoyote ile, lakini kwa Kagambo Bashaha hilo halikuwa gumu.
Usiku wa Januari 18, 2012, alijivua utu na kumuua mama yake, Rebeka Fares baada ya kumtuhumu kukataa kumuonesha baba yake, licha ya kumuomba kwa miaka kadhaa.
Akiwa mmoja wa watoto nane waliozaliwa na Rebeka kwa baba tofauti, Kagambo alilalamika kuwa mama yake aliwahi kumwambia hana baba na kwamba ni ‘wa hapa hapa tu.’
Baada ya kukamatwa na kushtakiwa, Kagambo aliongeza sababu nyingine iliyomkasirisha na kumsukuma kumuua mama yake, akidai marehemu ‘alimvunja nguvu za kiume’ kwa njia ya ushirikina baada ya kukataa kumwacha mkewe.
Kesi ya Kagambo ambaye hivi karibuni ameshindwa katika rufaa aliyokata kupinga adhabu ya kunyongwa inatoa picha jinsi imani za kishirikina zilivyoota mizizi katika jamii nyingi nchini, kiasi cha kuchochea chuki na hata mauaji.
Kwa upande mwingine inatoa fundisho kuhusu umuhimu wa kujenga familia ndani ya ndoa imara na athari ambazo jamii inaweza kupata pale wanawake na wanaume wanapoamua kuzaa kiholela.
Yalipoanzia
Kwa mujibu wa taarifa za upelelezi na rekodi za mahakama, kwa miaka mingi tangu afikie umri wa kujitambua, Kagambo alikuwa akimuomba mama yake ampeleke alipo baba yake mzazi.
Mara zote jitihada zake zilizimwa na majibu yasiyoridhisha na wakati mwingine kudhalilisha. Hali hiyo ilimsumbua kijana huyo na kumfanya amchukie mama yake.
Siku kadhaa kabla ya kumuua mama yake, Kagambo alifunga safari na kwenda alipoishi mama yake katika Wilaya ya Chato, mkoani Geita na kumwalika atembelee mahali alipoishi, ili pia amsaidie kuvuna pamba aliyokuwa amelima.
Bila kujua yatakayompata, Rebeka aliitikia wito wa mwanawe na kwenda naye hadi alipokuwa akiishi.
Siku ya tukio, Rebeka alikuwa amelala na mmoja wa watoto wake, Asha Moshi katika nyumba tofauti na muuaji. Kagambo aliamka usiku wa manane na kuichoma moto nyumba aliyolala mama na dada yake.
Baada ya kuhisi moto, Rebeka aliamka na kupiga kelele za kuomba msaada, lakini Kagambo aliyekuwa amelala nyumba ya pembeni hakuitikia wito huo.
Cha kushangaza, Kagambo aliitika baada ya muda mrefu kupita na alipofika kwenye mlango wa nyumba iliyokuwamo mama yake alimkuta mzazi wake mlangoni akiwa katika harakati za kujiokoa. Hapo alianza kumshambulia kwa panga kiasi cha kukaribia kutenganisha kichwa na mwili wake.
Rebeka alianguka na damu nyingi ilitiririka kutoka kooni kwake. Kwa bahati, kuna watu walisikia wito wake wa kuomba msaada na walipofika walimkuta ameshafariki dunia. Watu hao walimkamata Kagambo, walipomhoji alikiri kumuua mama yake. Wananchi walimfunga kamba na kumpeleka polisi.
Utetezi wake
Alipofikishwa mahakamani, alikiri tena kumuua mama yake. Aliieleza Mahakama Kuu, Mwanza kuwa alifanya hivyo kwa sababu marehemu alikataa kumweleza baba yake ni nani na aliishi wapi.
Alidai kuna wakati mama yake alimweleza hana baba na wakati mwingine alimjibu ‘wewe ni wa hapa hapa tu.’
Alidai pia mama yake hakuwa na uhusiano mzuri na mkewe na yeye hakuwa tayari kumuacha. Hali hiyo ilimfanya mama yake kumtishia ‘kumvunja nguvu za kiume’.
Katika kujaribu kulithibitisha hilo, Kagambo aliiambia mahakama kuwa baada ya kutishiwa hivyo alijikuta akishindwa kushiriki tendo la ndoa na mkewe na hata alipojaribu kwa wanawake wawili tofauti ilishindikana, hivyo alikasirika na kuamua kumuua mama.
Oktoba, 2017 Kagambo alihukumiwa adhabu ya kunyongwa baada ya mahakama kuridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi dhidi yake bila kuacha shaka.
Akata rufaa
Licha ya kuwa alikiri kosa, mwaka huo huo kijana huyo alikata rufaa kupinga adhabu ya kunyongwa.
Awali aliwasilisha sababu tatu za rufaa, lakini baadaye alizipunguza na kubaki moja baada ya kushauriana na wakili wake, Deocles Rutahindurwa.
Rutahindurwa aliishawishi mahakama iamini tabia ya mrufani kabla na baada ya mauaji iliashiria kuwa alipaswa kushtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia kuliko la kuua kwa makusudi.
Alifafanua chuki ya mrufani dhidi ya mama yake ilitokana na ukweli kuwa mama yake huyo alikuwa akikwepa kufanya hivyo kwa kutoa visingizio na majibu ya kudhalilisha.
Wakili huyo alisema uhusiano kati ya marehemu na mke wa mrufani haukuwa mzuri na kwamba marehemu aliwahi kueleza kuwa hakuwa tayari kuishi naye.
Rutahindurwa alidai uhusiano kati ya mrufani na mama yake ulishuka zaidi baada ya mama huyo kumtishia ‘kumvunja nguvu za kiume’ na kwamba baada ya maneno hayo mrufani alijikuta akishindwa kushiriki tendo la ndoa na mkewe na hata kwa wanawake wengine wa mtaani. Alimalizia kwa hoja kuwa kama jaji aliyemhukumu kifo angezingatia mazingira au mfululizo wa matukio yaliyozaa kesi hiyo, angemtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia na si kuua kwa kukusudia kama alivyoshtakiwa.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hemedi Halifani na Wakili wa Serikali, Lilian Meli walipinga hoja za rufaa wakidai shahidi wa pili wa utetezi aliwahi kusema kuwa alikuwa akimjua baba wa mrufani ambaye alikufa wakati mrufani akiwa na miaka 10 na kwamba mrufani alilijua hilo.
Kuhusu suala la marehemu kutoelewana na mkwe wake, Halifani alidai kuwa halikuwa na ukweli kwa sababu mrufani aliishi mbali na Chato alikoishi mama yake.
Kuhusu madai kuwa mama yake alimvunja nguvu za kiume, Halifani alikataa hoja hiyo na kuhoji aliwezaje kuthibitisha amekuwa hanithi ndani ya siku mbili baada ya kushindwa kushiriki tendo la ndoa na mkewe na wanawake wa mtaani. “Kwa kipimo chochote, hapakuwa na uthibitisho wa kisayansi kuthibitisha madai hayo. Hili suala la uhanithi ni kisingizio tu,” alidai wakili huyo.
Alisisitiza pia kuwa mrufani asingeweza kushtakiwa kwa kuua bila kukusudia kwa sababu hapakuwa na ushahidi kuwa mrufani alichokozwa na kwamba uchokozi huo ulimsababishia hasira ya ghafla kiasi cha kumuua mama yake.