Mbatia azidi kumpigania Mbowe




MWENYEKITI wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameiomba Serikali imfutie mashtaka ya ugaidi kiongozi mwenzake wa kisiasa wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake kwani haina afya kitaifa na kimataifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mbatia ametoa wito huo leo Jumatano, tarehe 8 Desemba 2021, akizungumzia hali ya kisiasa nchini, katika mdahalo wa kitaifa wa kujadili hali ya haki za binadamu katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Mwanasiasa huyo amesema, haipendezi kuona nchi inaadhimisha miaka 60 ya uhuru huku wanasiasa wengine wako mahabusu.

“Tufanye nini, naomba na ni raia yetu kesho tunafikisha miaka 60 ya uhuru lakini kuna wanasiasa wengine wako magerezani kwa makosa ambayo hayajengi heshima ya nchi,” amesema


 
Mbatia amesema “mtu kama ndugu yetu Mbowe yuko gerezani, inatupa heshima gani? Ndugu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria (Amon Mpanju), hebu tuwaombeni Serikali muyaondoe haya mashitaka ambayo hayana kichwa wlaa miguu ili tusherehekee kwa pamoja miaka 60 ya uhuru.”


James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi
Mpanju yupo kwenye mdahalo huo na ndiye aliyeufungua.

Mbatia ameisihi Serikali ifute mashtaka hayo ili kulinda utu wa Mbowe.


“Haya mashtaka hayaleti heshima ya nchi yetu, hatutaki kuingilia mambo ya mahakama na hatutakiwi kuingilia uhuru wa mahakamani, lakini hebu tufikirie kujenga hehsima na utu wa mtu,” amesema Mbatia.

Mbowe na wenzake ambao walikuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Adam Kasekwa, Mohammed Abdillah Ling’wenya na Halfan Hassan Bwire, wanasota rumande katika magereza ya Ukonga na Segerea, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka hayo.

Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, yuko rumande tangu tarehe 21 Julai 2021, alipokamatwa jijini Mwanza, kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam, na kuunganishwa katika kesi hiyo ya ugaidi.


Mbowe na wenzake, wanakabiliwa na mashitaka sita ya uhujumu uchumi, mahakamani hapo ambapo kesi hiyo inasikilizwa mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni, la kufadhili vitendo vya kigaidi, kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi ikiwemo kulipua vituo vya mafuta, sehemu zenye mikusanyiko ya watu wengi, kwa lengo la kuonesha Serikali imeshindwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Shitaka lingine linalowakabili ni la kupanga kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Kwa sasa kesi hiyo imesimama, ambapo itarejea tena tarehe 14 Desemba mwaka huu, kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Ling’wenya, yasipokelewe katika kesi ya msingi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad