Na Philemon Muhanuzi
Ligi Kuu ya England ni kisima kipana sana cha biashara za kimataifa. Miaka ya karibuni imekuwa ni ufahari fulani kwa taifa fulani kuwa na mwanasoka aliyecheza timu mojawapo ya ligi hiyo maarufu duniani.
Waingereza wameifahamu sukari waliyonayo na utamu wake wenye kujitofautisha.
Hauchezi tu Uingereza kama vile unacheza nchi nyingine ya Ulaya. Upo listi ya masharti ambayo unatakiwa uifuate ili mchezaji awe na sifa ya kucheza ligi hiyo.
Samatta aliifunga Liverpool akiwa Genk, mpaka dakika hii Uingereza wameshapita wanasoka kutoka mataifa 113 ya dunia hii. Mtanzania ni mmoja tu Mbwana Ali Samatta.
Ameweka rekodi ambayo waliomtangulia uwanjani hawakuweza kuifikia. Ameweka rekodi ambayo hawa wanasoka wa sasa hata hawaoti kuja kuifikia.
Wale wanaokwenda Morocco na Afrika Kusini kucheza soka kisha baada ya misimu miwili unawaona wakichezea timu ya Ligi Kuu Bara, huwezi hata kidogo kuwalinganisha na @samagoal77
Samatta amethubutu tena katika nyakati zilizojaa kukatishana tamaa. Nyakati zilizojaa maneno mengi ya kushindwa badala ya kujaribu mpaka kuweza licha ya vikwazo vingi njiani.’
Huyu kijana ni wa tofauti na vijana wengi wa rika lake. Takwimu za kidunia zinapozungumzwa hasa pale Uingereza lipo jina moja tu miongoni mwa maelfu ya nyota wa kigeni. Ni la Mtanzania Mbwana Samatta, apewe heshima yake akiwa bado wamoto.