Milango ya JELA Boda Haijafunguka..Kina Mbowe kula Krismasi, mwaka mpya gerezani




KIONGOZI wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, watasherekea sikuu ya Krismasi na mwaka mpya wakiwa gerezani jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ni baada ya kesi yao ya ugaidi iliyopo Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano jijini Dar es Salaam, kuahirishwa hadi tarehe 10 Januari 2022.

Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Joachim Tiganga ameahirisha kesi hiyo leo Jumatatu, tarehe 20 Desemba 2021. Ni baada ya mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja zao dhidi ya mapingamizi yaliyowekwa na utetezi.

Mapingamizi hayo yanahusu upokelewaji mali za mshtakiwa wa kwanza, Halfan Bwire Hassan, yatakapotolewa.


“Baada ya kupokea hoja za pande zote mbili, tumekubaliana kesi iahirishwe mpaka tarehe 10 Januari 2022, ambako tutakuja kusoma uamuzi. Hivyo, tunaahirisha mpaka tarehe 10 Januari, ambako itarudi kusikilizwa,” amesema Jaji Tiganga.

Kesi hiyo imeahirishwa, baada ya mawakili wa pande zote mbili kuendelea kuvutana dhidi ya upokelewaji wa mali hizo.

Mvutano huo uliibuka Ijumaa, tarehe17 Desemba 2021, baada ya shahidi wa nane wa Jamhuri, askari polisi Jumanne Malangahe, kuomba kuzitoa mali hizo, kama kielelezo cha ushahidi wake, ambapo mawakili wa utetezi, waliweka mapingamizi juu ya suala hilo.


Mali hizo ni baadhi ya vifaa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), zinazodaiwa kukamatwa nyumbani kwa Hassan, maeneo ya Yombo Kilakala, Dar es Salaam, tarehe 10 Agosti 2020, baada ya SP Malangahe kufanya upekuzi.

Upande wa utetezi waliweka mapingamizi juu ya upokelewaji wa mali hizo, huku wakitaja hoja za kisheria, ikiwemo iliyodai shahidi hakujenga msingi ulioonesha mlolongo wa utunzwaji na upokelewaji wake, mahakamani hapo (Chain of Custody).

Hoja nyingine zilidai, shahidi na mali hizo hazina uwezo wa kupokelewa kisheria, huku nyingine ikidai mali hizo hazikujumishwa katika mwenendo wa mashtaka (Committal Proceeding), uliyofanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kabla ya kuhamishiwa mahakamani hapo.

Leo upande wa Jamhuri kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, ameiomba mahakama iitupe hoja iliyodai shahidi hajaonesha mlolongo wa utunzwaji mali hizo, kwa kushindwa kutoa daftari ‘note book’ chenye taarifa ya alichokifanya wakati wa ukamataji mali hizo, akidai haina uhusiano na ombi la shahidi.


Wakili Kidando amedai, shahidi huyo ameweza kuonesha mlolongo wa utunzwaji wa mali hizo.

Hata hivyo, mawakili wa utetezi waliijibu hoja hiyo wakidai , shahidi na au mawakili wa jamhuri wakati wanajibu hoja zao, hawajaieleza mahakama namna SP Malangahe, alivyoonesha mlolongo wa utunzwaji na upokelewaji vielelezo.

Kwani hajaeleza nani aliyechukua vilelezo hivyo, kutoka katika chumba cha mashtaka, hadi kuvifikisha mahakamani hapo.

Kuhusu pingamizi lililodai mali hizo hazikuwasilishwa katika mwenendo wa mashtaka, Wakili Kidando ameiomba mahakama hiyo ilitupe akidai kwamba zilizkuwepo katika mwenendo huo.


“Hoja hii haina mashiko kisheria, sababu ushahidi huo sio mpya kama ambavyo mawakili wamedai. Ushahidi huo ulikuwepo tangu wakati wa committal proceedings zinafanyika na ushahidi huo ulisomwa mahakamani kwa mujibu wa kanuni ya 8 (2 ) ya kanuni za mahakama hii za 2016,” amedai Wakili Kidando.

Wakili Kidando amedai “na suala hilo linajumuisha katika ukurasa wa 32 na 33 wa proceeding za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Suala hili linaonekana mahususi kwenye ile list (orodha) hati ya ukamataji mali, inaonesha iko kwenye item 10.”

Licha ya jamhuri kutoa utetezi huo, mawakili hao wa utetezi wameendelea kupinga wakidai mali hizo hazikuwemo katika mwenendo wa mashtaka, kwani upande huo uliahidi utaziwasilisha baadae. Na kuwa hadi sasa hawajawasilisha orodha ya mali hizo, kwa washtakiwa au mawakili wao.

Wakili huyo wa Jamhuri, aliendelea kupangua mapingamizi hayo, akiiomba mahakama itupe mbali pingamizi lililodai shahidi wao hana uwezo wa kuzitoa mali hizo, kwa kuwa SP Malangahe alishindwa kuzithibitisha, kwa kuzitambulisha kwa mujibu wa sheria kwa kuweka alama za kipekee.

Wakili Kidando amedai shahidi alizitabulisha kwa ufasaha, kupitia alama alizokuwa anazitaja.


“Mh jaji ni submission (wasilisho) yetu kwamba, lebeling aliyoifanya shahidi namba nane inajitosheleza na inakidhi vigezo vilivyotajwa katika chapter (kurasa) namba tatu, paragraph (aya) ya 3.8 ya muongozo wa usimamizi wa vielezo wa mahakama,” amedai Wakili Kidando.

Hata hivyo, mawakili wa utetezi walipinga majibu hayo, wakidai shahidi alishindwa kuweka alama za kipekee zinazothibitisha kuwa mali hizo ndizo alizozikamata tarehe 10 Agosti 2020, baada ya kufanya upekuzi nyumbani kwa Hassan.

Pia, walidai alama hizo aliziweka baada ya kuzikama na kuwa mashahidi waliohusika katika upekuzi huo hawakushuhudia alama hizo.

Kwa upande wa pingamizi lililodai jina la eneo yaliyopo makazi ya mshtakiwa Hassan, ambako upekuzi huo ulifanyika, lilitofautiana katika hati ya ukamataji mali na ushahidi wa shahidi huyo.

Wakili Kidando amedai halina mashiko kwani shahidi wakati anatoa ushahidi wake, alifafanua eneo hilo liko maeneo ya Kilakala wilayani Temeke na sio Kilakala mkoani Morogoro kama ilivyodaiwa na ipande wa utetezi.

Pia, Wakili Kidando aliiomba mahakama hiyo alitupe pingamizi dhidi ya upokelewaji wa daftari lililodaiwa kuwa na taarifa mpya kutokana na kuonekana na baadhi ya karatasi zilizobanwa na pini.

Akidai kuwa halina mashiko kwani taarifa hizo sio ushahidi mpya, ulishasomwa tangu wakati wa mwenendo wa mashtaka.

Mbali na Mbowe na Hassan, washtakiwa wengine katika kesi hiyo, iliyoko katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, ni Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad