Mtu mmoja amefariki baada ya kupigwa na radi huku wengine 48 wakikosa makazi katika kijiji cha Huruma kata ya Kwanyama wilayani Tandahimba baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha na kuezua paa za nyumba zao
Akizungumza baada ya kufika katika kijiji hicho mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Patrick Sawala amesema mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali imeleta madhara makubwa katika kijiji hicho.
Ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuimarisha ulinzi wa wanachi hao na mali zao katika kipindi hiki ambacho wameanza kurekebisha makazi yao.
"Hili eneo limekuwa lilikumbwa na athari za mvua na upepo mara kwa mara mnatakiwa kuimarisha nyumba zenu. Tunatoa pole kwa wafiwa na kaya zote 48 zilizokutwa na madhara haya tutaimarisha ulinzi ili kihakikisha kuwa mnakuwa salama nyie na familia zenu," amesema Sawala.
Diwani wa kata hiyo Hamza Barakali amesema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko kutokana na mvua hiyo kuleta maafa kwa mwananchi wake.
"Mvua ilinyesha kubwa na iliambatana na upepo mkali na kusababisha mtu mmoja kufikwa na umauti, naungana na wananchi wa kata yangu nitasimamia mazishi na kuungana na wananchi wote ambao eneo lao limeathirika."
"Kwaweli inasikitisha nimepita kwenye nyumba zilizofikwa na madhara kweli nimetokwa na machozi sio jambo rahisi vyakula, malazi makazi yote yanahitajika ili wananchi hawa waweze kirudi katika hali zao za kawaida," amesema Barakali