Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Mathew Mkingule amebainisha umuhimu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji wa jeshi hilo na mafanikio yake katika ulinzi wa mipaka ya nchi, lakini akatoa ujumbe mkali wa onyo kwa maaskari wa jeshi hilo.
Mnadhimu huyo wa Jeshi alitoa ujumbe huo wa onyo kwa askari hao jana usiku wakati wa hafla ya kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, iliyofanyika katika viwanja vya makao makuu ya Kamandi hiyo Kigamboni.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mnadhimu Mkingule ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, amewataka askari hao kukumbuka na kuzingatia kiapo chao na kuwa wazalendo kwa nchi, na kuwatahadharisha kujiepusha na kutumiwa na watu wengine.
Mnadhimu Mkingule amewataka kuweka mbele maslahi ya umma katika kulitumikia Taifa na kumtii Rais wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu na si kumsikiliza yeye pekee na si mtu mwingine.
"Kumbukeni kiapo chenu. Mliapa mchana ili na ndege washuhudie. Mmeapa kulitumikia Taifa, kuweni wazalendo, muweke mbele maslahi ya umma badala ya maslahi yenu maana maslahi ya umma ni makubwa kuliko maslahi binafsi.", amesema Mnadhimu Mingule na kusisistiza:
"Mtiini Rais na Amiri Jeshi Mkuu, msikilizeni yeye maana pia mmeapa kumtii na kumlinda. Msisikilize sauti za watu wengine maana zitawapoteza."
Bila kufafanua kwa undani, Mnadhimu Mkingule amesisitiza tahadhari yake kwa askari hao kujiepusha kuwasikiliza na kutumiwa na watu wengine akisema kuwa wakishapata matatizo watu hao wanawaacha wanahangaika wenyewe.
Akizungumzia kuanzishwa kwa Kamandi hiyo, Mkingule amesema kuwa ni Kamandi muhimu sana kwani ilianzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyrere, Desemba 6, 1971 kwa lengo la kukamilisha jukumu la Ulinzi wa mipaka ya nchi katika maeneo yote yaani nchi kavu,angani na majini.
Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwake kamandi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa akiyataja kuwa imeweza kupambana na kudhiti uhakifu mbalimbali kama vile uharamia na uvuvi haramu baharini na katika maziwa, kuzuia usafirishaji wa binadamu na uingizaji wa dawa za kulenya.
Mkingule amesema kuwa dawa za kulevya ambazo ni tatizo kubwa linaloathiri Taifa moja ya njia kubwa za kupitishia dawa hizo ni baharini lakini Kamandi hiyo imeza kupambana na tatizo hilo kwa mafanikio makubwa.
Hata hivyo ametoa wito kwa maafisa na viongozi wa Kamandi hiyo kusisitiza mafunzo kwa askari akisema kuwa mafunzo ni jambo muhimu Sana katika jukumu lao la ulinzi wa mipaka.
Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Rear Admiral Michael Mumanga amewapongeza wakuu wa Kamandi hiyo waliomtangulia kwa mchango wao akisema kuwa mafanikio ambayo Kamandi hoyo imeyapata yanatokana na msingi waliouweka wao
Awali Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa Kamandi hiyo, Commodore Msafiri Hamis wakati akifunga michezo mbalimbali iliyofanywa na vikosi mbalimbali vya Kamandi hiyo kama sehemu ya maadhimisho hayo, aliwataka waandaaji wa maadhimisho hayo kuhakikisha kuwa .maadhimisho yajayo yanakuwa bora zaidi.