Kwa kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AC Milan jana, staa wa Liverpool, Mohamed Salah, ameifikia rekodi ya Cristiano Ronaldo ya kupasia nyavu katika mechi saba mfululizo za ugenini kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ronaldo, staa wa Manchester United kwa sasa, aliiweka rekodi hiyo kuanzia mwaka 2013 hadi 2014, wakati huo akiwa mchezaji wa vigogo wa La Liga, Real Madrid.
Mara ya mwisho kwa Salah kutofunga bao katika mechi ya ugenini ilikuwa dhidi ya Ajax mwaka jana, mchezo ambao hata hivyo Liver walishinda bao 1-0.
Aidha, bao la jana lilikuwa la 20, ikiwa ni kwa msimu wa tano mfululizo kumuona mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 akifikisha idadi hiyo.