Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ametangaza kuchangia kiasi cha Bilioni 2, ikiwa ni ya awali katika kuhakikisha Simba inajenga Uwanja wake ambao utatumika katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki.
Mohamed Dewji ametangaza kutoa mchango huo wa awali kufuatia kupokea maoni mengi ya wana Simba wenzake wakimshauri kujenga uwanja wao na wako tayari kuchangia ili kufanikisha ujenzi huo.
''Nimepokea maoni mengi ya wana Simba wenzangu wakishauri tujenge uwanja wetu na wako tayari kuchangia ili tufanikishe ujenzi huo. Naomba kuweka wazi kwamba nimepokea maoni hayo kwa mikono miwili''
''Naomba Bodi ya Simba kukaa na kuja na utaratibu wa haraka ili jambo hili lianze utekelezaji. Kwa kuanza naahidi kuchangia Tsh.2 bilioni. Nawaomba wanasimba tucheangie sote''Mohamed Dewji.
Hivi karibuni aliyekuwa mshauri Mkuu wa Mohamed Dewji akiwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Simba,Crecentius Magori aliandika katika mitandao yake ya kijamii kushauri ujenzi wa uwanja wao kufuatia C.E.O wao, Barbra Gonzalez kuzuiwa kuingia katika dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam katika dabi ya Kariakoo ya tarehe 11 mwezi 12,2021.
Barbra alizuiwa kuingia Uwanjani kufuatia kuingia uwanjani katika eneo la VVIP akiwa na watoto ambao inadaiwa hawakuwa na kadi zenye majina yao.