Mtanzania Ericson Temu amekuwa mwamuzi wa kwanza kutoka nchini Tanzania kuchezesha mchezo wa soka nchini England.
Temu mwenye umri wa miaka 26 anatarajia kuchezesha mechi nyingine ya Ligi ya England baada ya kuchezesha mchezo wake wa kwanza kama mwamuzi wa kati kwa umaridadi mkubwa wikendi iliyopita aliposimamia pambano la vijana chini ya umri wa miaka 23 baina ya Charlton Athletics na QPR.
Temu mkazi wa mkoani Arusha alisoma elimu yake ya msingi na sekondari katika Shule ya St.Jude iliyopo mkoani Arusha kabla ya kuelekea nchini Mauritius kwa masomo ya juu na baadaye nchini England.
Akiwa St.Jude nchini Tanzania alianza kusomea kozi za awali za urefa zilizokuwa zikitolewa na Chama cha Soka Mkoa wa Arusha kwa nyakati tofauti.
Temu amesema ndoto yake ni kuchezesha ligi kuu ya soka nchini Uingereza na kwa kiwango alichokionyesha katika mchezo wake wa kwanza anaamini hilo litawezekana ndani ya muda mfupi huku chama cha marefarii kikiahidi kumpangia michezo mingine.