UONGOZI wa Klabu ya Yanga umeweka wazi kuwa uko tayari kumshusha kikosini hapo kiungo mshambuliaji wa
zamani wa Simba raia wa Zambia, Clatous Chama katika dirisha hili la usajili ikiwa tu kocha wa timu
hiyo, Nasreddine Nabi atapitisha jina lake.
Kwa muda mrefu sasa Yanga imekuwa ikihusishwa kufukuzia saini ya Chama ambaye taarifa za ndani kutoka klabu anayoichezea ya RS Berkane ya Morocco, zinaeleza kuwa hana furaha katika timu hiyo kutokana na kukosa nafasi
ya kucheza na kutozoea mazingira, hivyo yupo kwenye mipango ya kuvunja mkataba.
Dirisha dogo la usajili wa wachezaji linatarajiwa kufunguliwa rasmi leo Jumatano ambapo pamoja na Yanga, inaelezwa kuwa klabu yake ya zamani ya Simba ipo kwenye mpango wa kumrudisha.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga, Rodgers Gumbo alisema: “Kuhusiana na usajili wanyota wa kimataifa hatutarajii kufanya mabadiliko makubwa sana ya kikosi kwenye dirisha hili dogo la usajili.
“Tuna nafasi mbili lakini mpango wetu ni kusajili mchezaji mmoja tu ambaye atakuja kuziba pengo la
Yacouba Songne, ambayeripoti za kitabibu zinaeleza atakuwa nje mpaka mwishoni
mwa msimu.
“Hivyo tunatarajia kusajili kiungo mmoja mshambuliaji, kuhusu usajili wa Chama hilo liko chini ya kocha wetu
mkuu Nasreddine Nabi, ambaye alipata nafasi ya kumuona Chama akicheza hapa nchini na kama ataona
hilo ndilo chaguo sahihi la kuziba nafasi ya Yacouba basi tutahakikisha tunamsajili.”