Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) ikishirikiana na Jeshi la Polisi inawashikilia mawakala 18 na wamiliki sita wa mabasi wanaodaiwa kulangua tiketi kwa abiria.
Desemba 21, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waita alifanya ziara ya kushtukiza katika Stendi ya Magufuli jijini hapa na kubaini baadhi ya mabasi yamepandisha nauli tofauti na iliyopangwa na Latra. Wapo waliotozwa hadi Sh60,000 kwa safari waliyopaswa kulipa kati ya Sh35,000 na Sh45,000 kutoka Dar.
Mwita alisema abiria hao waliandikiwa nauli halisi ya mahali wanakokwenda, hivyo akaiagiza Latra kufuatilia kwa umakini suala hilo na watakaobainika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Jana Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe akiwa katika Stendi ya Magufuli kufuatilia mwenendo wa mabasi yanayofanya safari zake kwenda mikoani kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka alithibitisha watu hao kushikiliwa na polisi, ingawa hakuwa tayari kuwataja wamiliki hao zaidi ya kusema ni wale walioshindwa kuwasimamia mawakala wao.
“Tumeona ni wamiliki, siyo mawakala walioghushi tiketi na tumewauliza walikuwa wapi hadi tiketi zikawa mtaani. Watapumzika kwanza na tutakutana mahakamani. Natoa wito kwa wengine wasiendelee na ujinga kama huu.
“Tumekuja hapa tangu saa 10 alfajiri tunafuatilia kila kona kujua kinachoendelea, wanaofanikiwa sawa, lakini tukikupata hatuna huruma na wewe. Tupo kila mahali Msata, Morogoro, Iringa, Dodoma, Mwidu na maeneo mengine kwa saa 24, ikitoka taarifa unakamatwa, sasa utakimbilia wapi?” alisema Ngewe.
Abiria wengi wanaopatikana kuanzia saa tatu asubuhi na kuendelea alisema wanakwenda mikoa ya Dodoma na Morogoro na Latra imeruhusu mabasi kuondoka hadi saa moja kuelekea Morogoro na saa 11 jioni kwenda Dodoma ili kurahisisha usafiri kwa abiria.
“Sasa hivi tuna mabasi 10 yaliyofanyiwa ukaguzi, endapo kutatokea dharura, basi yatakuja kupakia abiria waliozidi na kuondoka. Abiria wanaokwenda Morogoro wameongezeka baada ya mabasi yao kupunguzwa na kuruhusiwa kwenda mikoa ya kaskazini,” alisema Ngewe.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus John alisema “nawapongeza Latra kwa sababu kulikuwa na utaratibu mbovu wa basi kuandikiwa faini wakati wakala na wapigadebe wameuza gari kwa Sh50,000 halafu wameandika tiketi Sh30,000. Muda mwingine ni ngumu kubaini.”