ALIYEKUWA mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Christian Makonda, anatarajiwa kutinga mahakamani, kesho Ijumaa, tarehe 3 Desemba 2021, ili kujibu kwa nini asishitakiwe kwa matumizi mabaya ya madaraka. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Kesi dhidi ya Makonda, imefunguliwa na Saed Kubenea, mwandishi wa habari mashuhuri na mbunge wa zamani wa Ubungo (Chadema), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Maombi hayo yamesajiliwa mahakamani kwa Na. 7/2021 – Miscellaneous Criminal Application – yanatarajiwa kutajwa kesho, mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Aron Lyamuya.
Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo mahakamani, Kubenea anaeleza katika kesi hiyo, kwamba Machi mwaka 2017, Makonda alivamia kituo cha televisheni cha Clouds, jambo ambalo ni kuingilia maudhui ya matangazo ya televisheni nchini na kinyume cha sheria za nchi.
Aidha, kitendo cha Makonda, kuvamia kituo hicho majira ya saa nne usiku, akiwa na askari waliovaalia sare za kijeshi, ni matumizi mabaya ya madaraka.
Katika tukio hilo, Makonda – mwanasiasa aliyetikisa katika kipindi cha utawala wa Rais John Pombe Magufuli – alivamia Clouds, majira ya saa nne usiku, akiwa ameongozana na maofisa wanne waliokuwa wamevalia sare tofauti za majeshi ya ulinzi na usalama; watatu kati yao, wakiwa wamebeba silaha za moto.
Kwa mujibu wa rekodi zilizopo mahakamani, Kubenea amewasilisha maombi hayo ya kutaka kumshitaki Makonda, chini ya kifungu cha 99 (1) cha Sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai, Sura ya 20, ambapo kumeelekezwa kuwa pale wanaopaswa kushitaki wakishindwa kufanya hivyo, mtu binafsi anaweza kuchukua jukumu hilo.
Washitakiwa wengine, ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Paul Makonda, ambayo ni maombi mchanganyiko Na. 7 ya mwaka 2021.
Maombi hayo yamewasilishwa kwa njia ya wito maalum (Chamber Summons) na hati ya kiapo, akiomba kufungulia mashitaka Makonda. Yamefunguliwa tarehe 24 Novemba 2021.
Kubenea katika maombi hayo, ameambatanisha hati ya mashitaka (Charge Sheet), yenye makosa mawili, matumizi mabaya ya madaraka, chini ya kifungu cha 96 ya Kanuni ya adhabu (Penal Code), Sura ya 20 na kosa la pili, kuingilia mawasiliano ya Kieletroniki.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashitaka, kosa hilo la pili, linaangukia kwenye sheria ya Kieletroniki na Posta la mwaka 2010, ambayo ni sheria Na. 3 na kwenye hayo maombi, kumeambatanishwa ripoti ya Kamati Maalum iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye.
Ripoti ya Nape iliyochunguza tukio la kuvamiwa Clouds, ilimtia hatiani Makonda na kupendekeza kwa mamlaka yake ya uteuzi, kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi huyo.
Hata hivyo, mapendekezo yote ya Kamati ya Serikali hayakutekelezwa na kwamba muda mfupi baada ya Nape kumaliza kusoma ripoti yake kwa waandishi wa habari, Rais Magufuli, alimfuta kazi.