Ndo hivyo Chama kufuata nyayo za Okwi



HABARI za kurejea nchini kwa kiungo fundi raia wa Zambia, Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ zimepamba moto kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo ambapo timu mbalimbali inakitumia kuimarisha vikosi vyao.

Klabu za Simba na Yanga ndio ambazo zimekuwa zikihusishwa na kiungo huyo ambaye anaichezea RS Berkane ya Morocco inayonolewa na Florent Ibenge.

Simba inaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupata huduma ya Chama kutokana na kipengele cha kimkataba (wa Chama) ambacho kinaeleza ikiwa fundi huyo atataka kurejea tena Tanzania basi chaguo la kwanza ni timu hiyo.

Kipengele hicho kinaelezwa kuwa kiliwekwa wakati ikifanyika biashara ya uhamisho wa Chama kutoka Simba na kwenda Morocco kuungana na kocha wa zamani wa AS Vita na timu ya taifa ya DR Congo, Ibenge ambaye alivutiwa naye.

Chama anatajwa kutokuwa na furaha huko Morocco na yote hiyo inatokana na kutokuwa chaguo la kwanza la Ibenge kwenye kikosi chake.

Mbali na Chama ambaye muda wowote anaweza kurejea Simba hawa hapa nyota wengine wa kigeni ambao walirejea kwenye klabu zao za awali ambazo walizichezea nchini, akiwemo Heritier Makambo.

HERITIER MAKAMBO

Huu ni msimu wake wa kwanza, Makambo tangu arejee nchini akitokea Horoya AC ya Guinea, Yanga iliamua kumrejesha mshambuliaji huyo mwanzoni mwa msimu huu baada ya timu yao kuwa na changamoto kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Kutokana na kile ambacho alikifanya Makambo akiwa na Yanga kwenye awamu yake ya kwanza kuichezea timu hiyo ambapo alitupia mabao 17 kwenye ligi, iliaminika kuwa moja kwa moja anakuja kuwa tiba ya kile ambacho kilikuwa kikiwasumbua kwa msimu uliopita wa 2020/21.

Licha ya kutokuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Nasreddine Nabi, kutokana na kufanya vizuri kwa mshambuliaji mwenzake, Fiston Mayele, Makambo amekuwa akionyesha makali yake pindi apewapo nafasi.

EMMANUEL OKWI

Anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa kigeni wenye heshima kubwa mbele ya mashabiki wa Simba na soka la Tanzania kwa ujumla.

Hivi karibuni, aliyekuwa nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema kuwa Okwi ndiye mshambuliaji wake bora wa muda wote kukabiliana naye wakati akicheza soka la ushindani. Amefanya makubwa Okwi katika awamu zake zote tatu ambazo ameichezea Simba kwenye miaka ya 2010-13, 2014-15 na 2017-2019.

Baada ya kuachana na Al Ittihad ya Misri, Okwi alikuwa akihusishwa kurudi tena Simba kwa awamu ya nne lakini dili hilo liligonga mwamba na badala yake mshambuliaji huyo wa Kiganda aliamua kujiunga na Kiyovu ya Ligi Kuu Rwanda.

ABASIRIM CHIDIEBERE

Unaweza kusema kuwa huyu jamaa ni kama Mtanzania vile kwani maisha yake yamekuwa hapa kwa miaka mingi tangu alipotua kwa mara ya kwanza, 2013 akitokea kwao Nigeria, alianza kuichezea Stad United.

Chidiebere alifanya vizuri akiwa na Stand United kabla ya chama hilo kushuka daraja na baadae akaibukia, Coastal Union ya Tanga lakini akarejea tena Stand kabla ya 2017 kwenda Zimbabwe ambako aliichezea CAPS United.

Baada ya mkataba wake kumalizika huko Zimbabwe aliamua kurejea zake Tanzania ambapo hadi sasa bado anacheza soka la kulipwa akiwa na Mbeya City.

BOBAN ZIRINTUSA

Mganda, Boban Zirintusa ni miongoni mwa wachezaji ambao wamecheza ligi nyingi za mataifa mbalimbali, uzoefu wake ni mkubwa maana aliwahi kucheza Uganda (kwao), Zimbabwe,England, Afrika Kusini na Zambia.

Si mchezaji mgeni Tanzania kwani aliwahi kuichezea kwa mara ya kwanza Mtibwa Sugar,2009 hadi 2013 ambapo alitimka zake kabla ya msimu huu kuamua kurejea, Manungu. Siku chache zilizopita alipachika mabao matatu kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Tunduma United.

HARUNA NIYONZIMA

Aliondoka nchini kwa heshima kubwa tofauti na wachezaji wengi wa kigeni ambao wamepita Yanga, wananchi walimuandalia siku maalum na kumfanyia tafrija fupi ya kumuaga fundi huyo ambaye amaichezea Yanga kwa miaka mingi.

Haruna ambaye siku chache zilizopita alitunukiwa cheti cha ukocha huko nchini kwao Rwanda ambako bado anacheza soka huku akijiendeleza, ni kati ya wachezaji wachache wa kigeni ambao walipata mafanikio akiwa na miamba ya soka la Tanzania kwa maana ya klabu za Simba na Yanga.

Kwa mara ya kwanza, Haruna kutua nchini ilikuwa 2011 akitokea APR ya nchini kwao, Rwanda aliichezea Yanga kwa miaka sita kabla ya kwenda Simba na baadae AS Kigali kisha kuamua kurejea tena Jangwani, mwaka jana, 2020.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad