Ndugai: Hakuna sababu za kubishana na mamlaka



 
Ndugai: Hakuna sababu za kubishana na mamlaka
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amesema hakuna sababu za kubishana na mamlaka juu ya mapendekezo ya kuhamisha eneo la Ikulu ya Chamwino kwenda Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Akizungumza wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Dodoma (RCC) alisema tayari Mamlaka zimepitisha mapendekezo ya kuhamisha Kata tatu za Wilaya za Chamwino zilizopendekezwa kuingia Jiji la Dodoma za Chamwino Ikulu, Msanga na Buigiri.

“Hatuna sababu za kubishana na mamlaka hili tulipokee, kwanza tulikubali huwezi kuchukua mipaka ya Ikulu ukaileta Mjini , Kata zikihamia Mjini zinaleta ukubwa wa Jiji hiyo ni fursa tuwashauri wakichukua kata tatu Jiji ligawanyike kuwe na Jiji na manispaa,” alisema.

Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa alisema pia hata mapendekezo ya wajumbe kutoka Wilaya ya Chamwino igawanywe na kuwa na Halmashauri mbili lina mashiko kutokana na jiografia ya Chamwino . Mbunge wa Jimbo la Mvumi, Livingstone Lisinde alisema pendekezo la kuhamisha Kata tatu za Chamwino kuingia Jiji mapendekezo yao ni kupata Wilaya mpya ya Mvumi. Alisema Mvumi ina Kata 22 na ina wingi wa watu.


 
“ Hoja yetu baada ya Kata tatu kuingia Jiji mapendekezo yetu Chamwino tupate Wilaya mbili za Mvumi na Chilonwa. Alisema jiografia ya Chamwino ni kubwa na wananchi wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za jamii lakini kukiwa na Halmshauri mbili kutarahisisha upatikanaji wa huduma.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa, White Zuberi alisema Baraza la mawaziri lilikaa na kufanya maamuzi ya Kata tatu kuingia Jiji la Dodoma kwa ajili ya heshima ya Ikulu jambo hilo linatakiwa kuungwa mkono. Alisema Pamoja na hayo lazima liwe na mapendekezo ya Chamwino kuwa na Halmashauri mbili.

Hivi karibuni mkutano wa dharura wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma lilipitisha kwa kauli moja kuhamisha eneo la Ikulu ya Chamwino kwenda Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi. Akihitimisha mkutano huo wa dharura Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa Baraza la Madiwani limepitisha mapendekezo ya Kata tatu za Chamwino, Buigiri na Msanga kuingia Jiji la Dodoma.


Mapendekezo mengine ni kugawanya Jimbo la uchaguzi la Dodoma mjini, kuongeza tarafa moja na kuunda halmashauri mbili za Manispaa. Ikumbukwe kuwa sehemu kubwa ya eneo la Ikulu ipo upande wa Jiji la Dodoma kwa ukubwa wa hekta 2,249 sawa na ekari 5,557 kati ya jumla ya hekta 3,429 sawa na ekari 8,469.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad