Mume wangu tulikutana chuo, mimi nikiwa na miaka 20, yeye 21. Tukaanza kuishi pamoja kama mke na mume.
Tulikuwa tukiandika majarida mitandaoni ndo tunapata pesa ya kujitunza wenyewe, na ndo pesa nilimsomeshea mdogo wangu kwani mama alikuwa mgonjwa na tuliishi maisha duni sana. Mimi na mume wangu tulilelewa na mama pekee.
Ikatokea kozi aliyokuwa anasoma mwenzangu kuwa na shida, wote waliokuwa wanaisoma wakasimamishwa masomo kwa muda, na kulikuwa na kesi mahakamani. Lakini baadae ilirudishwa na wenzake walirudi shule lakini yeye hakurudi, kwahiyo hakumaliza chuo. Nafikiri pia pesa aliyokuwa akipata wakati huo ilimfanya asirudi chuo.
Me nilisoma nikamaliza. Sikukaa muda mrefu nikapata kazi. Huku mwenzangu kazi ya uandishi ilianza kusuasua, mara asiandike, kwahiyo me nikawa ndo nalipia matumizi yote nyumbani.
Nikasema itakuwa wakati muafaka kuzaa, labda tukipata mtoto atapata moyo wa kutafuta kwa bidii. Tukapata mtoto, lakini mambo yalikuwa yaleyale. Mimi huku nako niliendelea kuchakarika, kuanzisha biashara n.k.
Nilichogundua, mwanaume akiwa hana kitu chake/pesa yake anakuwa hajiamini kabisa.
Basi hapo akaanza ku cheat. Me mwenyewe kusema ukweli nili cheat pia, maana unaenda kazini unakutana na wanaume wachapakazi unarudi nyumbani unamuona mwenzako kakaa tu unawaza huyu vipi! Tukaenda hivyo baadae baada ya kugunduana tukakaa kuongea, tukasameheana tukakubaliana tuanze upya.
Lakini mambo yalikuja kuwa mabaya zaidi, alininyanyasa kihisia na mwishowe alikuwa akinipiga.
Tukaamua tuachane, hiyo ni baada ya miaka tisa ya kuwa pamoja. Akaondoka nyumbani. Kwakweli nilivurugwa sana. Nilihisi amenipotezea muda mwingi, kanikuchua Nina miaka 20 kaniacha nina 29.
Nikawa mtu wa pombe. Narudi nyumbani saa nane usiku na asubuhi naenda kazini yani sijui niliwezaje kufanya kazi. Nikawa na mahusiano kadhaa, mmoja hadi aliniingiza kwenye utumiaji wa madawa.
Baada ya miaka miwili ya hayo maisha nikasema huku nje sio! Bora kurudi kwa shetani ninayemjua. Na hilo lilikuwa kosa kubwa sana nililofanya. Basi tukarudiana na huyo mume wangu, ambaye bado alikuwa Hana kazi.
Hapo mimi nikawa nimeokoka. Nikasema haya mahusiano tusirudishe yalivyokuwa, tuanze upya kama Mungu anavyotaka. Basi tukajiunga kwenye darasa la wanaotarajia kuingia ndoani.
Tukapanga siku ya harusi. Nikawa nampa pesa alipie vitu hadi mahari, maana huwa tunaambiwa kumfichia mwanaume aibu unampa yeye hela ndo atoe.
Nilijinunulia Pete nikampa, siku mmoja tulienda mgahawani akanivalisha. Kwahiyo mitandaoni mtu anaona tu nimevalishwa Pete hajui story.
Nilikuwa very desperate kwakweli, na nilifanya hivyo kwasababu kwanza niliona maisha huko nje sio, na pili nilitaka mwanangu awe na familia iliyokamilika. Harusi ilinimalizia akiba yangu yote.
Basi tukafanya harusi, tukaanza kugombana huko huko honeymoon! Kurudi nyumbani tena manyanyaso yalizidi.
Nikiri kuwa wote na mume wangu tuna tatizo la hasira, tena me wananiitaga mdomo pistol maana maneno yanayonitoka nikikasirika ni kama pistol.
Alikuwa akininyanyasa kihisia kwa kunikumbusha makosa yangu ya zamani kila mara. Vipigo vilizidi hadi mama yangu ambaye alikuwa amekuja kuishi na sisi akasema hataki kuishi hapo arudishwe kwao.
Tulijaribu counseling, pastor wetu alijitahidi sana kusaidia ndoa yetu. Unakuta baada ya misa anatuita, ananiambia ukirudi nyumbani wewe fanya hivi na hivi lakini tukifika nyumbani unaibuka ugomvi, ananipiga hadi majirani wanaamka.
Mtoto naye niliitwa shuleni nikaambiwa anaongea sana kuhusu kupigana, kwamba anaogopa anataka kumlinda mama yake lakini hajui amlindeje. Wakamuanzishia therapy shule. Na kazini kwangu pia kuna huduma ya counseling nilimpeleka.
Alipata therapy kwa miezi kadhaa na alianza kupona maana aliacha kuuliza kama nitarudiana na baba na siku moja therapist wake alimwmbia achore picha ya familia yake, akajichora yeye na mimi tu.
Sasa hivi tunaweza kuangalia picha za baba yake tukamuongelea vizuri. Kabla ilikuwa akiona picha ya baba anaanza kulia. Inauma sana kuona mwanao anaumia, bora ingekuwa kaumia mwilini ungesema ngoja nimpake hiki, lakini kihisia hujui ufanye nini!
Baba yake niliachana naye baada ya kujua kuna mwanamke mwingine, ex wake.
Ndo nikasema haiwezekani juhudi zote nazofanya, nimejitahidi kubadilika, kuomba msaada kanisani, nikawa mtu wa sala asubuhi mchana jioni ni kuomba tu Mungu aiponye ndoa yangu, nalipia bills zote, yeye kutwa kunikumbushia makosa yangu ya nyuma, halafu kumbe ana mwanamke mwingine!!! Nisingejua kuhusu huyo mwanamke nafikiri bado ningekuwa naye. Nikamwambia aondoke. Hiyo ni miezi minne tu baada ya harusi.
Wakati tunafunga harusi binafsi nilikuwa na furaha. Lakini niliwahisha mambo, hatukukaa kufikuria kwanini mahusiano yalishindikana mara ya kwanza. Kwakweli kufanya harusi haiondoi matatizo kwenye ndoa au mahusiano yenu.
Niliumia sana kuachana naye, hasa baada ya kufanya harusi kubwa miezi minne tu iliyopita. Nilikuwa silali. Nilikuwa na mawazo ya kujiua. Nikaanza kupata anxiety attacks.
Nikaenda hospitali nikaanza kupewa dawa na kufanya therapy kwa miezi kadhaa. Mawazo ya kujiua yamepotea. Nimekubali kuwa nimejitahidi kadri ya uwezo wangu kuokoa ndoa yangu.
Nikajiunga na divorce classes, yanasaidia kukabiliana na hisia zinazokuja na talaka kama Uoga, hasira, Upweke. Ni ngumu kujifunga huko tena baada ya miezi minne tu ya ndoa, unawaza utaambiwa na watu Mungu hapendi talaka. Sawa hapendi talaka lakini anampenda yule mtaliki.
Najihisi nimekuwa mtu bora zaidi, Najua nilipokosea, Najua ninachotaka kwenye mahusiano.
Sisemi kwamba ikitokea shida udai talaka. Pigania ndoa yako. Ipiganie mpaka hata Mungu akishuka aseme kweli ulifanya hiki na hiki na hiki. Ukiona imefika mwisho, achana nayo. Talaka sio mwisho wa maisha.
Mimi naona mume mzuri ni mwanaume anayemjua na anayeongozwa na Mungu kwasababu huyo atajua jinsi ya ku behave. Awe mchapakazi na Anayechukulia maagano ya ndoa kwa uzito.
Tazama VIDEO: