Okwi, Chama na Luis Wapewe Heshima Yao Simba

 


NA PHILEMON MUHANUZI

NIMEKUWA nikivifuatilia vikosi vya Simba vya miaka mingi sasa, kila usajili mpya unapofanyika nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu, na nimewaona watatu ambao viwango vyao bado vipo juu kulinganisha na vya wengine. Wanakuja wachezaji na kuondoka pale Msimbazi lakini vya kwao ni kama vinastahili tuzo maalum.


Nawazungumzia Emmanuel Okwi, Clatous Chama na Luis Miquissone. Hawa watu walistahili mamilioni waliyolipwa pale Msimbazi. Okwi alikuwa ni balaa. Mshambuliaji mwenye uwezo wa kucheza kama winga wa kushoto na pia akacheza kama namba kumi anayesimama nyuma ya mshambuliaji wa mwisho. Popote mpange lakini majibu yake utayapata muda wote akiwa anatafuta goli la ushindi.


Chama hana kasi lakini amejaliwa akili na ufundi wa hali ya juu. Mpira utapelekwa kwake ukiwa ni pasi ya juu lakini atakavyoipokea na kuanza kupiga danadana unaweza kudhani ni suala dogo analifanya. Aliulainisha uchezaji mzima wa Simba. Asipopiga pasi ya mwisho basi atamchagua golikipa.


Luis Miquissone ni winga mwenye kulazimisha mabeki wafanye makosa. Anawafuata huku akiwapunguza. Hapunguzi kasi ya shambulizi. Mpira ukimfikia kwake anaupokea na kuliendeleza shambulizi kama alivyoupokea.


Lile goli alilowafunga Al Ahly pale Uwanja wa Taifa ni la kiwango cha dunia. Kila litakapotazamwa kama sehemu ya marudio ule utamu wake hautakuja kupungua.


Hao ni wanasoka watatu ambao wameacha mapengo ndani ya Simba. Hawa wa msimu huu wengi wao ni vijana kiumri na kiuchezaji. Watakuja kuchanganya lakini mpaka muda huo ufike ile nafasi ya heshima ipo kwa hao watatu niliowataja.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad