Pablo apewa rungu Simba



WAKATI kikosi cha Simba kimewasili jijini Dar es Salaam juzi usiku kimyakimya kutoka Bukoba na kuelekea kambini huku wachezaji wao wakienda moja kwa moja kufanyiwa vipimo vya afya, uongozi wa klabu hiyo kwa sasa unasubiri ripoti ya Kocha Mkuu, Pablo Franco kupendekeza maeneo anayohitaji kuboreshwa.

Wachezaji wa Simba, kutoka kulia; Aishi Manula, Jonas Mkude na Hassan Dilunga, ni miongoni mwa kikosi cha wachezaji 23 ambao walisafiri na timu kwenda Bukoba kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar, ambayo hata hivyo haikuchezwa kutokana na nyota wengi wa 'Wekundu wa Msimbazi' hao kuugua. PICHA: MAKTABA
Jumamosi iliyopita Simba ilishindwa kucheza mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba baada ya wachezaji wake 16 kuugua mafua na kukohoa na homa, (Season Influenza) hali iliyoelezwa ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hata hivyo, juzi timu hiyo ilirejea Dar es Salaam kimyakimya na kuingia kambini moja kwa moja tayari kujiandaa na mechi ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC itakayopigwa Desemba 24, mwaka huu, katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Thierry Hitimana, alisema baada ya kurejea juzi usiku wachezaji wote wameingia kambini na jana kupatiwa vipimo kwa ajili ya kuangalia afya zao kuelekea mechi ijayo dhidi ya KMC FC.

Alisema hali ya wachezaji wao haiko sawa na hawataendelea na mazoezi hadi hapo watakapopata majibu ya vipimo ili kugundua tatizo na baada ya hapo ndipo wataendelea na programu zao.


 
“Tumeingia jana (juzi) usiku Dar es Salaam, wachezaji wote wako kambini na hatuwezi kuendelea na programu ya mazoezi hadi hapo tutakapopata majibu ya vipimo kuona tatizo la wachezaji wetu, baada ya hapo tutaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao,” alisema Hitimana.

Kuhusu usajili, Hitimana alisema hadi sasa hakuna mapendekezo yoyote yaliyotolewa kutoka benchi la ufundi, na kwamba viongozi wanasubiri ripoti kutoka kwa Pablo ili kuanza kuboresha timu yao.

Alisema bado hawajakaa na bosi wao (Pablo) kupitia ripoti na ana imani kila kitu kitakuwa sawa kwa sababu muda wa kufanya usajili bado upo hadi Januari 15, mwakani.

Naye Mwenyekiti wa Wanachama wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, alisema wako makini katika kila kitu na suala la usajili wanasubiri ripoti kutoka benchi la ufundi linaloongozwa na Pablo.

Alisema watafanya maboresho kwa kusajili wachezaji kulingana na mahitaji ambayo yanapendekezwa na kocha wao huyo kwa ajili ya michezo iliyopo mbele yao ikiwamo kutetea ubingwa wao na kufikia malengo yao kwa msimu huu.

"Tutafanya maamuzi magumu katika dirisha dogo la usajili kupata wachezaji bora kama ambavyo kocha (Pablo) atahitaji kwa ajili ya kuifikisha timu yetu katika malengo ya kufanya vizuri na kutwaa makombe katika mashindano ya ndani na nje ya Tanzania," alisema Mangungu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad