KUNA uwezekano mdogo kwa chama tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumvua uanachama wa chama hicho, mbunge wa kuteuliwa na Rais, Humphrey Polepole na kisha kupoteza ubunge wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa kutoka makao makuu ya CCM, mjini Dodoma na Bunge zinasema, ni vigumu kumfukuza Polepole, kutokana na hatua ya uongozi wa Bunge, kuwakingia kifua wabunge 19 waliovuliwa unachama ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
“Huwezi kumfukuza Polepole, kisha kina Mdee (Halima James Mdee) na wenzake, wakaendelea kubaki bungeni. Hivyo basi, njia sahihi ya kushughulikia jambo hili, ni kumuacha yeye na wale wabunge wa Chadema,” ameelezaa kada mmoja mwandamizi ndani ya chama hicho tawala.
Amesema, “lakini bila sakata la Mdee, Polepole angeliwa kichwa kama ambavyo Sophia Simba, alifukuzwa uanachama na kupoteza ubunge wake.”
Kupatikana kwa taarifa kuwa kuna uwezekano mdogo kwa Polepole kupoteza uanachama wake ndani ya CCM, kumekuja wakati chama hicho tawala, kilifanya vikao vyake vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC), mjini Dodoma juzi na jana Jumamosi.
Mikutano yote miwili – CC na NEC – ilikuwa chini ya mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, kupatikana kwa taarifa kuwa “Polepole hafukuziki,” kumekuja wakati tayari Kamati ya maadili ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekwisha kumhoji yeye, Askofu Joseph Gwajima na Jerry Silaa.
Askofu Gwajima ambaye ni mbunge wa Kawe na Silaa wa Ukonga, wao wamehojiwa pia na kamati ya kinga, maadili na madaraka ya Bunge na kupewa adhabu ya kutohudhuria mikutano kadhaa vya Bunge.
Wabunge wote watatu kwa maana ya Polepole, Askofu Gwajima na Silaa, wameitwa tena na kamati kuu ya CCM juzi, kwenda kuhojiwa juu ya tuhuma zinazowakabili.
Mdee na wenzake 18, walifukuzwa uanachama wa Chadema na Kamati Kuu ya chama hicho, kufuatia kutuhumiwa na kupatikana na hatia kwenye makosa ya kujipeleka bungeni bila idhini ya chama na kughushi sahihi ya Katibu Mkuu, John Mnyika.
Walituhumiwa pia na kutiwa hatiani kwenye makosa ya usaliti, uchonganishi, ubinafsi, upendeleo na kujiapisha kuwa wabunge wa Chadema, kinyume cha taratibu na maelekezo ya vikao vya chama.
Mdee aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), alituhumiwa kutenda makosa hayo, huku akijua wazi kwamba anachokitenda, ni kinyume na Katiba, Kanuni na miiko ya uongozi ndani ya kilichokuwa chama chake.
Naye Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alikitaka chama hicho kujieleza kwa nini CC, iliwavua uanachama Mdee na wenzake, tarehe 27 Novemba 2020.
Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa CC, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu Mkuu Bawacha, Grace Tendega; aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti baraza hilo (Bara), Hawa Subira Mwaifunga.
Katika orodha hiyo, wamo pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; aliyekuwa katibu mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat; aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.
Wengine, ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.
Jingine linalotajwa kuwa kitamuokoa Polepole, ni kuingizwa kwenye chama hicho na kupewa madaraka makubwa ya uongozi na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Hayati John Pombe Magufuli.
“Akifukuzwa leo, watu watasema, atashughulikiwa kwa kuwa Magufuli hayupo tena. Kwa hiyo, atashughulikiwa kwa njia nyingine, ambayo haitakuwa na madhara kwa chama,” ameeleza mtoa taarifa huyo.
Wakati hali ikidaiwa kuwa hivyo ndani ya CCM, juzi Ijumaa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), iliamuru kusimamishwa kwa muda, kipindi cha “Shule ya Uongozi,” kinachoendeshwa na Polepole.
Katika uamuzi wake, TCRA imeeleza kuwa imetoa masharti kadhaa ya kipindi hicho kufunguliwa, ikiwamo kuwa na watumishi wenye taaluma ya uandishi na utangazaji wa habari, ili kuleta tija katika vipindi vyake.
Kamati imesema, televisheni hiyo haina watumishi wenye taaluma, jambo ambalo linasababisha kuwapo kwa ukiuka sheria, misingi na kanuni za taaluma ya habari na utangazaji.
Mbunge huyo ndiye mmiliki wa televisheni ya Online ya “Humphrey Polepole Online” iliyokuwa inaendesha kipindi hicho.
Kamati hiyo imemuagiza Polepole kuhakikisha vipindi vyake vyote vinazingatia sheria, kanuni na misingi ya uandishi na utangazaji wa habari pamoja na masharti ya leseni yake.
Baada ya kutimiza masharti hayo, TCRA imeeleza kuwa kituo hicho kitatoa taarifa kwake, ambapo ikijiridhisha kuwa maelekezo yote yamezingatiwa, kipindi cha Shule ya Uongozi kitarejea na kuwa chini ya uangalizi wa mamlaka hiyo kwa miezi sita.
“Humphrey Polepole Online,” kimepewa onyo kali baada ya kuthibitika kuwa maudhui ya kipindi chake ni ya upotoshaji yanayoweza kusababisha taharuki kwa wananchi.
Maamuzi hayo yametangazwa baada ya kumhoji Polepole ambaye ndiye mmiliki wa televisheni hiyo na mwendeshaji wa kipindi husika kinachoruka kupitia mitandao ya kijamii.
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Polepole alisema, aliutarajia na kwamba kufuatia hatua hiyo, anatarajia kukaa na timu yake ya wasaidizi ili kuona namna ya kujinasua katika adhabu aliyopewa na mamlaka hiyo.
Akiongea kwa kujiamini, Polepole amejinasibu kuwa kazi ya kusema kweli nchini bado ina safari ndefu na yeye hatokata tamaa maadam anachokifanya kinalinda masilahi mapana ya nchi, watu, mamlaka ya nchi na CCM.
Alisema mamlaka hiyo, ilimpa nafasi ya kusikilizwa na kwamba “kazi ya kusema kweli ina safari kidogo,” na anadhani kwa yeye ambaye ni “mwanachama wa CCM kwa imani na ninayeamini katika kusema kweli daima, bila kuweka chembe ya fitina ndani yake… na ninayemini katika ahadi nyingine ya mwanachama wa CCM inayosema nitafanya jitihada kujielimisha na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote, kwangu mimi hii ni mitihani midogo.”
Katika nyakati tofauti, Polepole amekunukuliwa na televisheni yake hiyo akisema, virusi vya corona -19, vimetengenezwa na kampuni kubwa ili kuuza chanjo na kujipatia fedha, madai ambayo hajaweza kuyathibitisha na bila kutoa nafasi kwa mtaalam wa afya kutoa ufafanuzi wakati akiendesha kipindi chake.
Kamati ya maudhui ya TCRA imesema, madai hayo yamedhoofisha jitihada za mapambano dhidi ya ugoinjwa huo. Jingine ambalo ametuhumiwa nalo, ni kusema deni la taifa limekuwa kubwa na kuwataka viongozi kutoa ufafanuzi, lakini akashindwa kutoa nafasi kwa viongozi wenye mamlaka ya kuzungumzia jambo hilo, kwenye kipindi chake.
Kamati imethibitisha kuwa mawaziri wa fedha walitoa ufafanuzi bungeni kuhusu deni na kusema kuwa ni himilivu.