Polepole na Sabaya Wawe Funzo, Mtego wa PANYA Umewapitia

 


Nakumbuka kuna kisa cha mtego wa panya ambacho nilisimuliwa miaka mingi iliyopita ambacho leo hii ningependa kuwashirikisha wale wasiokijua.


Hapo kale kulikuwa na familia ambayo ilikuwa inasumbuliwa sana na panya waliokuwa wakiharibu nguo, kula nafaka, vyakula na kufanya uharibifu mbalimbali. Familia hiyo ilipochoshwa na kadhia hiyo ikakubaliana ikanunue mtego wa panya.


Wakati mjadala huo ukiendelea, panya akiwa na rafiki zake (jogoo, mbuzi na ng’ombe) walikuwa wakiusikia kwa kina na ulipoisha waliwaambia panya umezidi uharibifu sasa umetafutiwa mtego.


Panya aliwaambia kuwa mtego huo ukija wasaidiane kuuharibu kabla haujaleta madhara kwa kuwa mtego huo huwanasa waliomo na wasiokuwamo (hunasa panya na viumbe wengine).


Baada ya mtego kuwekwa usiku akaingia nyoka ndani ya nyumba na akabanwa, wakati akihangaika kujinasua mwenye nyumba alisikia purukushani akaamua kwenda kuangalia mtego. Alipoinama! Hamad akagongwa na nyoka kichwani akapiga kelele.


Watu walipokuja wakamuua nyoka, lakini mwenye nyumba akiwa hoi akakimbizwa hospitali ambako umauti ulimfika. Mtego wa panya ukasababisha vifo vya mwenye nyumba na nyoka.


Usiku huo kwa kuwa watu walikuwa wachache pale msibani na mboga haikuwapo ilikakubalika achinjwe jogoo, wakati akienda kuchukuliwa panya alimwambia nilikuambia mtego wangu hunasa waliomo na wasiokuwamo.


Siku ya pili kwa kuwa watu walikuwa wengi ikakubalika achinjwe mbuzi na siku ya tatu ambayo ndiyo yalikuwa maziko ya mwenye nyumba alichinjwa ng’ombe.


Mtego wa panya ukawa umewanasa na kusababisha vifo vya nyoka, mwenye nyumba, jogoo, mbuzi na ng’ombe. Kama panya angesikilizwa vifo hivyo visingetokea.


Hapa nchini wakati wa utawala wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, watu walilalamika sana juu ya kuminywa kwa uhuru wa maoni, watu kujieleza, utungaji wa sheria kandamizi na zinazokiuka misingi ya utawala bora.


Wakati huo watu wakipiga kelele, mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole alikuwa akishangilia ndani ya ‘V8’ na kuzunguka nchi kueleza utendaji uliotukuka wa Serikali ambao unainyoosha nchi kutoka kwa wahuni, hivyo kuwataka watu wengine watulie.


Sasa hivi Polepole analalamikia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), CCM na wakubwa wengine Serikalini kwa kumziba mdomo asikosoe madudu yanayofanyika.


Polepole anasema uhamishaji wamachinga ulifanyika sivyo ndivyo na ulikiuka haki za watu wengine. Leo hii Polepole hataki kuzibwa mdomo wakati akiikosoa Serikali, hataki apewe amri za kunyamazishwa anapotumia uhuru wake wa Kikatiba wa kueleza yasiyomfurahisha.


Leo hii ‘Shule ya uongozi’ aliyokuwa akiitoa kupitia televisheni mtandao aliyoisajili imezuiwa na TCRA, Polepole sasa anajua sheria zilizotumiwa na mamlaka hiyo ni kandamizi lakini zilitungwa wakati yeye akiwa na nafasi ya kushawishi ndani ya chama zisitungwe. Kanaswa na mtego wa panya.


Hakuona sababu ya kufanya ushawishi wa sheria hiyo isipitishwe kwa kuwa aliona haimhusu, kwa kuwa yeye ndiye msemaji wa chama tawala, sasa mambo yamebadilika ndiyo anaona ubaya waliokuwa wakiuona wenzake wakati ule.


Hivyo hivyo kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ambaye amefungwa miaka 30 kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.


Wakati akiwa madarakani aliambiwa aache ubabe na kuumiza watu kwa kisingizio cha kutumwa kazi maalumu na wakuu wake wa kazi. Kila alichoambiwa aliwaona wanaomwambia hawamtakii mema na wanamuonea kijicho kwa nafasi aliyonayo.


Hata wale waliomwambia kuwa wadhifa huo ni sawa mtego wa panya, aishi vizuri na watu hawakuwa wamekosea, bali waliona mbali na walishahisi shimo lake siku akiondolewa madarakani.


Linapofanyika jambo baya bila kujali linamgusa nani kila mmoja wetu awe wa kwanza kulizuia au kuliondoa. Asipofanya hivyo siku linaweza kufanyika kwake au kwa watu wanaomhusu na asipate msaada atakapopiga kelele za kusaidiwa.


Polepole na Sabaya ni mifano hai ya hivi karibuni. Waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Fedrick Sumaye nao baada ya kuhama CCM walielewa kilio cha wapinzani kuwa wanaonewa.


Walielewa nguvu ya polisi katika kuwadhibiti wapinzani, wanajua amri za polisi vinavyominya demokrasia ya vyama vya upinzani. Walitamani sheria zifuatwe lakiwa walikuwa nje ya ulingo wa kurekebisha hilo.


Walipokuwa viongozi waliona hizo ni kelele zisizowahusu, lakini walipotoka waliona zinawahusu.


Augustine Mrema alihama kutoka CCM kwenda NCCR-Mageuzi. Huyu hakuwa mtu mdogo serikalini, amewahi kuwa Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Kazi, Waziri wa Mambo ya Ndani. Huyu alipata kila heshima kutoka kwa askari wa juu mpaka wa chini, alisafishiwa barabara ili apite kuwahi majukumu.


Haikufikiriwa kuwa siku moja Mrema angepigwa mabomu ya machozi na polisi aliowaongoza, hakuwahi kufikiri polisi hao ndio wangezuia msafara wake na kuwatawanya wafuasi wake. Hili ni funzo kubwa kwetu sote.


Walioko madarakani wasitunge sheria kwa mahitaji ya sasa au kuwadhibiti kina fulani, tusitunge kwa lengo la kudhibiti au kunyoosha eneo au watu fulani, bali tutunge kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. Tusiache mtego wa panya…

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad